Na Mwandishi Wetu
WOTE tunakubali kwamba mimea na maua kwa ujumla, inafanya mandhari ya nyumba iwe nzuri na ya kuvutia.
Hata hivyo, usalama wa watu na wanyama wanaofugwa unapaswa kupewa uzito unaostahili pindi mtu anapopanga kutengeneza bustani.
Hii ni kwa sababu yapo maua yanayovutia kwa mwonekano pindi yanapochanua, lakini yanaweza kusababisha hasara ya muda mrefu ikiwamo kuharibu ardhi hadi kusababisha kifo kwa watu na wanyama.
Mimea hii inatajwa kuwa na kiwango kikubwa cha kemikali zenye sumu zinazoweza kusababisha shida ya tumbo, matatizo ya kupumua na maradhi ya moyo.
Mtaalamu wa bustani, Luciana Massawe, anasema hatua ya kwanza ya kuchukua ni kufanya utafiti wa aina ya maua kabla ya kuyapanda nyumbani kwako.
“Ikiwa tayari umepanda maua haya kwenye bustani yako, napendekeza uyaondoe haraka. Utaokoa maisha ya wale uwapendao pamoja na ekolojia kwa ujumla,” anasema.
Baadhi ya mimea anayotaja ni Butterfly Bush, linalovutia sana vipepeo na wadudu wengine wachavushaji. Linatajwa kuwa hatari kwa kuharibu ardhi.
Ua lingine ni Caladium, yenye majani yenye kuvutia kutokana na umbo la moyo. Lingine ni Crocus Autumn, maua haya mawili nayo yanatajwa kuwa na kiwango kikubwa cha sumu aina ya calcium oxalate, inayoweza kusababisha muwasho wa ngozi, kuvimba midomo, ulimi na kuleta kichefuchefu, kutapika na kuharisha, kama italiwa na wanyama.
UNAWEZA KUTOA MAONI KUHUSU HABARI HII KUPITIA 0753333330