Na Mwandishi Wetu
UNASUMBULIWA na nyoka au wadudu wakali? Je, nyumba yako iko kwenye mazingira ambayo nyoka anaweza kuingia? Usigope. Ipo mimea ambayo inaweza kuwafukuzia mbali na kukuhakikishia usalama.
Licha ya kwamba baadhi ya mimea inastawi vizuri zaidi kwenye maeneo ya baridi, lakini mchaichai, vitunguu (swaumu na maji), ulimi wa mama mkwe na marigold, inaweza kustawahi katika mazingira yote.
Mimea hii inatajwa kuwa na uwezo wa kufukuza nyoka kutokana na harufu kali inayomkosesha raha nyoka, hivyo kumfanya asisogee kwenye eneo au bustani yako.
MARIGOLD
Wataalamu wanaeleza kuwa harufu yake na mizizi ya marigold huwafukuza nyoka.
Mkulima katika kijiji cha Onana, Kata ya Kibosho Magharibi, mkoani Kilimanjaro, Peter Massawe, anasema aina hiyo ya ua huwafukuza pia wadudu waharibifu wa mazao ya mbogamboga na nyoka.
“Shambani kwangu nimeyapanda sehemu tofauti tofauti ili kulinda mazao. Ni mazuri ukipanda nyumbani kwa sababu unafukuza nyoka,” anasema.
Anataja mmea mwingine ambao pia umetajwa na wataalamu wa kilimo kuwa ni mchaichai.
Wataalamu wanaeleza kuwa mchaichai unapokatwa, hutoa harufu kali ambayo huwasumbua nyoka.
“Hata kama nyoka ameshaingia kwenye eneo lako, ukiwa umevuna mchaichai ile harufu inamsumbua kwa hiyo ataondoka tu,” anasema.
Katika orodha hiyo, lipo ua la ulimi wa mama mkwe (snake plant), ambalo linaogopwa na mnyama huyo. Ni ua linalopaswa kupandwa katika kila nyumba kutokana na uwezo wake wa kuzalisha hewa safi ya oksijeni na kufukuza wadudu wasumbufu.
Mmea mwingine unaotajwa na wataalamu ni vitunguu maji na swaumu, ambavyo vinawafukuza nyoka kwa harufu yake.
“Nyoka ni wageni wasiokubalika katika mazingira ya nyumbani, ikiwa unajiuliza jinsi ya kuwazuia, mimea ambayo ni dawa asilia isiyo na kemikali, ni suluhisho salama zaidi,” anasema Massawe.
Anasema mimea hiyo ni rafiki wa mazingira, huleta harufu nzuri nyumbani na chakula kwa ajili ya afya.
Trending
- EPUKA MAUA HAYA NYUMBANI KWAKO
- FUKUZA NYOKA KWA MIMEA HII
- DARASA LA SABA KUPEWA UFADHILI
- MAENDELEO BENKI YATAJA ONGEZEKO LA FAIDA 2024
- BRELA, UDSM wawanoa wadau faida miliki ubunifu
- Utafiti kilimo, mifugo na uvuvi kutokomeza njaa
- NMB yaja na mwarobaini mikopo kausha damu
- TARI kuzalisha miche 100,000 ya parachichi msimu ujao