Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MAENDELEO benki imeendeleza historia yake ya kupata faida kwa miaka 10 mfululizo, kwa kupata faida ya Sh. bilioni 3.69 kabla ya kodi mwaka jana 2024, ukilinganisha na Sh. bilioni 2.63, mwaka juzi 2023.
Aidha, ongezeko hilo ni sawa na ukuaji wa asilimia 40, wakati faida baada ya kodi Sh. bilioni 2.83 na mapato halisi yatokanayo na riba yakiwa Sh. bilioni 10.84 ukilinganisha na Sh. bilioni 8.05 sawa na ukuaji wa asilimia 35, huku uwiano wa gharama kwa mapato ikifikia asilimia 61.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 03, 2025, mkoani Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Fedha wa benki hiyo, Nolasco Charles, amesema nidhamu ya utekelezaji wa mpango mkakati, ushirika na wateja pamoja na kujitolea kwa wafanyakazi katika utendaji kazi kumechangia ukuaji wa mapato na faida kwa mwaka jana.
Amesema mambo mengine yaliyoipatia Maendeleo benki matokeo mazuri ni pamoja na kuimarisha biashara ya mikopo na kwamba ukuaji wa kitabu cha mikopo umefikia Sh. bilioni 88.78 kwa mwaka 2024 kutoka bilioni 74.09, mwaka juzi 2023.
Amesema amana za wateja zimekua kwa asilimia 14 kutoka Sh. bilioni 90.79 mwaka 2023, hadi Sh. bilioni 103.73 mwaka 2024, huku mali za benki zikiongezeka kutoka Sh. bilioni 124.69 na kufikia Sh. bilioni 150.56 ikiwa ni ukuaji wa asilimia 21.
Amesema mtaji wa benki umeongezeka kwa asilimia 15 na kufikia Sh. bilioni 21.94 ambao unaipa sifa ya kuwa benki ya kitaifa na kufungua matawi nchi nzima.
“Benki inaendelea kurudisha faida kwa jamii kwani mwaka 2024 tulifanikiwa kutumia zaidi ya Sh. milioni 180 ikijumuisha tukio la mbio za hisani (Maendeleo Bank Marathon 2024), ambalo lilikusanya jumla ya Sh. milioni 140 ambazo zilikuwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa katika wodi ya watoto njiti katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya (KCMC), Kilimanjaro na ujenzi wa kituo cha watoto waliozaliwa na changamoto ya ulemavu wa akili cha Mtoni, Dar es Salaam” amesema Charles.
Charles ametaja malengo ya mwaka huu kuwa ni kuendeleza ukuaji wa benki kwa njia ya kidijitali kwa kufanya uwekezaji kwenye teknolojia.
Lengo lingine ni kuongeza mtaji wa benki kwa kufungua matawi katika mikoa ya Arusha, Dodoma na Mwanza na kuboresha kitengo cha huduma kwa wateja katika matawi yote kwa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa watumishi wote.
Tunatarajia kuanzisha bidhaa bunifu, rafiki zinazoendana na mahitaji ya wateja…ili kuongeza faida kwa mwaka kutoka Sh. bilioni 2.8 mwaka 2024 na kufikia Sh. bilioni nne mwaka 2025,” amesema. Mkuu wa Idara ya Biashara Maendeleo Benki, Emmanuel Mwaya (kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Idara ya Fedha wa benki hiyo, Nolasco Charles, wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari Februari 3, 2025, Dar es Salaam.