Sekta za kilimo, uvuvi na mifugo, zinafanyiwa utafiti wa kina, ili zitumike kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa yanayolenga kumaliza njaa ifikapo mwaka 2030.
Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi, Anna Makinda, ameyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya siku 14 kwa wadadisi na wasimamizi 178 wa kilimo kwa mwaka wa 2023/2024, yaliyofanyika katika Chuo cha Afya ya Msingi, mjini Iringa.
Amesema jukumu la wadadisi na wasimamizi hao litakuwa ni kukusanya na kuchambua takwimu sahihi za uzalishaji katika sekta hizo.
“Roho na uhai wa nchi unategemea takwimu sahihi. Takwimu hizi zitawasaidia wakulima kujua ni kiasi gani cha mbolea kinahitajika kwa shamba la ukubwa fulani na hivyo kuweza kubashiri mavuno.”
Amesema takwimu hizo zitasaidia kuongeza uzalishaji na kuwezesha nchi kufikia viwango vya kimataifa vya mipango ya uzalishaji.
Makinda amesema baada ya kukamilika kwa utafiti, jamii itaweza kufaidika na miradi ya maendeleo iliyopangwa, ambayo itazingatia mahitaji halisi yaliyobainishwa kupitia takwimu.
“Miradi itapewa kipaumbele kulingana na maeneo yenye uhitaji mkubwa zaidi,” amesema.
Mtakwimu Mkuu kutoka Zanzibar, Kasimu Salim Ally, amesema mafunzo kama hayo yanaendelea pia visiwani Zanzibar na akahimiza washiriki kutimiza wajibu wao ili malengo ya utafiti huo yatimie.
Awali, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Albina Chuwa, amesema takwimu za kilimo, uvuvi na ufugaji, zitasaidia kuweka sera bora za kukuza sekta hizo.
“Utafiti utaiwezesha serikali kupima hatua zilizofikiwa katika mapambano dhidi ya njaa kabla ya mwaka 2030,” amesema.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema takwimu watakazokusanya, zitasaidia kukuza sekta ya kilimo, uvuvi na ufugaji, kwa kuwa zitakazowezesha mipango ya maendeleo.
Trending
- BRELA, UDSM wawanoa wadau faida miliki ubunifu
- Utafiti kilimo, mifugo na uvuvi kutokomeza njaa
- NMB yaja na mwarobaini mikopo kausha damu
- TARI kuzalisha miche 100,000 ya parachichi msimu ujao
- BBT YAANZA KUZAA MATUNDA KWENYE UVUVI
- MAREKANI YATOA BIL 60/- KUIMARISHA USALAMA WA CHAKULA
- BOT YAONYA APP ZA MIKOPO MTANDAONI, YAPIGA MARUFUKU UDHALILISHAJI
- VIJANA, WANAWAKE WAPEWA MITAJI WEZESHI MILIONI 101/-