Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kituo cha Tengeru kimeanza kuzalisha miche 100,000 ya parachichi aina ya HASS, ambayo itauzwa kwa wakulima kwa bei elekezi.
Taarifa iliyotolewa na TARI kwa umma kupitia mitandao yake ya kijamii leo, imeeleza kuwa miche hiyo itakuwa bora na taasisi hiyo itaifikisha kwa wakulima katika msimu ujao wa kilimo kupitia ofisi za halmashauri.
DONDOO MUHIMU KUHUSU HASS
Watafiti wameeleza kuwa, Hass ni miparachichi inayozaa mapema kuanzia miaka miwili na nusu hadi mitatu tangu kupandwa na haina magonjwa na wadudu kutokana na uandaji bora.
Sifa nyingine ni vikonyo vya kubebeshea huchukuliwa kwenye miti halisi ya Hass, soko la uhakika kutokana na kuuzika ndani na nje ya nchi, matunda yake yana soko kitaifa na kimataifa hivyo ina soko la uhakika na parachichi la Hass kuwa na madini mengi ya calcium, magnesium, vitamini A, B, C, D, E na K, yanayoboresha afya na lishe.
“Tunda lina nyama yenye ubora wa juu, haina nyuzinyuzi na ina kiwango cha mafuta cha asilimia 18 hadi 23. Matunda huweza kukaa kwa muda kwa wiki mbili hadi tatu baada ya kuvunwa, hivyo kurahisisha usafirishaji wa mbali ukilinganisha na aina nyingine za parachichi,” imeeleza taarifa ya TARI.