Benki Kuu ya Tanzania imetoa mwongozo kwa wakopeshaji wa kidigitali na kupiga marufuku wakopeshaji mtandaoni kutumia lugha za kudhalilisha, kuchapisha taarifa za waliokopeshwa mtandaoni au kutuma jumbe kwenye namba zilizopo katika simu ya aliyekopeshwa.
Muongozo wa Agosti 2024, unakuja wakati ambao kuna ongezeko la taasisi mbalimbali zinazotengeneza App za kukopesha; ambazo baadhi zinalalamikiwa kwa utendaji usiofaa.
Mathalani tarehe 04 Juni 2024, baadhi ya wabunge walilamika kuhusu kuungwa kwenye makundi ya WhatsApp ambapo vitambulisho vya watu wanaosemwa kuwa na madeni vimekuwa vikitumwa, huku pia wakituma jumbe fupi kwa namba za watu wa karibu wa waliokopeshwa.
Mwongozo huo wa BoT, unataka mkopeshaji kidigitali kusajiliwa na Benki Kuu na pia mfumo wa kidigiti anaoutumia lazima uwe salama katika utumiaji.
MARUFUKU YA MWONGOZO HUO
1. Kutumia vitisho, vurugu au njia zingine za kumuumiza aliyekopeshwa katika marejesho.
2. Kutumia lugha za matusi kwa mteja au wadhamini wa mteja au namba zingine kwenye simu yake kwa nia ya kumdhalilisha.
3. Kuangalia katika simu ya mteja namba zingine za simu kwa ajili ya kuwatumia meseji watu wengine, mteja anaposhindwa kulipa katika muda au asipolipa.
4. Kutuma taarifa binafsi za mteja katika mitandao kwa ajili ya kumdhalilisha.
5. Kupiga simu au kutuma meseji kwa namba zingine zilizopo kwenye simu ya mteja.
6. Mtoa mikopo hataruhusiwa kutumia mifumo ya ukopeshaji kuangalia namba za simu katika simu ya mteja, kuangalia simu alizopiga au kupokea. Pia hataruhusiwa kuangalia: meseji, picha, mitandao yake ya kijamii, email, mafaili au Applikesheni mbalimbali kama njia ya kumtambua mteja au kuendelea kuwa na mahusiano naye kama mkopeshaji.
7. Mkopeshaji hataruhusiwa kuzitoa taarifa binafsi zilizokusanywa na kuchakatwa Tanzania kwa watu au taasisi zilizoko nje ya Tanzania, labda kwa ajili ya matengenezo na maboresho ya jukwaa la kukopesha.
8. Wakopeshaji mtandaoni hawaruhusiwi kuendesha jukwaa la kukopesha kabla ya kupata idhini ya BoT, pia wakitaka kufunga hawatatakiwa kufanya hivyo bila kupata idhini ya Benki Kuu.
Trending
- BRELA, UDSM wawanoa wadau faida miliki ubunifu
- Utafiti kilimo, mifugo na uvuvi kutokomeza njaa
- NMB yaja na mwarobaini mikopo kausha damu
- TARI kuzalisha miche 100,000 ya parachichi msimu ujao
- BBT YAANZA KUZAA MATUNDA KWENYE UVUVI
- MAREKANI YATOA BIL 60/- KUIMARISHA USALAMA WA CHAKULA
- BOT YAONYA APP ZA MIKOPO MTANDAONI, YAPIGA MARUFUKU UDHALILISHAJI
- VIJANA, WANAWAKE WAPEWA MITAJI WEZESHI MILIONI 101/-