Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), imewataka Watanzania kuchangamkia uwekezaji katika maeneo hayo ili wazalishe bidhaa zinazokidhi soko la nje ili kuiongezea nchi fedha za kigeni.
Hayo yameelezwa na Kaimu Meneja wa uhamasishaji wa EPZA, Nakadongo Phares, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kwenye Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nane-nane yanayoendelea kwenye viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.
“Tuko hapa Nane-nane kutoa elimu kwa wananchi, lakini pia kuelezea fursa zilizopo za kupata maeneo maalum katika fursa za uwekezaji wa viwanda vinavyozalisha kwa ajili ya kuuza nje ya nchi,” amesema Nakadongo.
Amesema EPZA ina programu ya kumwezesha mwekezaji mzawa na mgeni, kupata leseni itakayompa nafasi ya kuwekeza kwenye eneo maalum hususani ujenzi wa kiwanda kwa lengo la kuuza nje kwa asilimia 80 na ndani asilimia 20.
Aidha, amesema mwekezaji anaruhusiwa kuuza bidhaa zote alizozalisha nje ya nchi kwa asilimia 100, ikiwa atapenda kufanya hivyo.
Amefafanua kuwa leseni anayoipata mwekezaji inamuwezesha kupatiwa eneo maalum lililoboreshwa tayari kwa uwekezaji.
Ametaja baadhi ya maeneo hayo ni yaliyopo Bagamoyo mkoani Pwani, Manyara, Mtwara na Tanga; na katika mikoa mingine.
“Kwahiyo ninawahamasisha wawekezaji wetu wa ndani kutumia fursa hizi kwenye maeneo yetu maalum ya uwekezaji wa viwanda. Tusiache hii fursa ikatumiwa na watu wa nje,” amesema Nakadongo.
Mamlaka hiyo inatoa leseni za aina tatu kwa wawekezaji ambazo ni ya ujenzi (SEZ Developer License), kwa ajili ya wawekezaji wa kujenga miundombinu ya SEZ/EPZ katika maeneo yaliyobainishwa.
Nyingine ni ya kuanzisha kiwanda (EPZ/SEZ operator License), kwa ajili ya wawekezaji wanaozalisha bidhaa katika Maeneo Maalum ya uwekezaji SEZ/EPZ yaliyokamilika kujengwa na ile ya kutoa huduma za maji, umeme, mawasiliano na huduma zafdha, katika maeneo hayo.