Na Restuta James
UKISASA wa vitu vingi duniani unahamia kwenye kuboresha vitu vya asili kuanzia aina ya ujenzi wa nyumba hadi mapambo yake.
Leo tunaangazia mapambo ya ndani yanayotokana na vitu asilia kama ukili, katani, migomba na kamba za aina mbalimbali ambazo miongo kadhaa iliyopita zilionekana kama vitu vya watu masikini.
Kama inavyoonekana pichani, ubunifu wa kazi za mikono zilizonakishiwa kwa rangi ni pambo la nyumba za ‘matajiri’ ndani na nje ya Afrika.
Wataalamu wa mapambo ya ndani wanaeleza kuwa sanaa ya ubunifu ndio inaosababisha kazi za mikono kuteka soko la kimataifa la urembo na mapambo.
Anastazia Jonathan, anasema upambaji wa kutumia ubunifu unatokana na vitu vya asili ambavyo havijapitishwa viwandani, unaongeza thamani ndani ya nyumba na kuifanya ya kisasa zaidi.
“Kinacholeta utofauti ni mpangilio wa rangi na uasili unaobakia wakati wa kukamilisha pambo husika…rangi si lazima zipakwe kwenye pambo pekee, unaweza kupaka kadhaa na vingine vikabakia kwa uasili na vikapangwa vizuri ukutani vinapendeza sana,” anasema.
Anafafanua kuwa: “Mapambo haya yanafaa ukiweka na kioo lakini ukiyaweka mengi kwenye ukuta mmoja. Ni muhimu sana ukazingatia ukuta unaoonekana zaidi.”
Anasema pambo la ukuta linapendeza likiendana na sofa akitolea mfano wa kutumia foronya za batiki kwenye mito ya sebuleni.
Anasema rangi ya ukuta nayo inapaswa kuzingatiwa kabla mtu hajaamua kutumia pambo la asili au batiki.
Anatoa rai kwa wabunifu na wajasiriamali kuzalisha bidhaa zinazoendana na soko kwa kuwa zina uhakika wa kupenya kwenye masoko makubwa ndani na nje ya nchi.