Na Restuta James, Morogoro
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Hashil Abdalllah, amewahimiza waandishi wa habari kuelimisha umma umuhimu wa kurasimisha biashara, ili waweze kunufaika na fursa zitakazowawezesha kukuza mapato.
Dk. Hashil ameyasema hayo leo Juni 18, 2024, mjini Morogoro alipokuwa akifungua mafunzo ya waandishi wa habari wanaoripoti kutoka jiji la Dar es Salaam.
Amesema kupitia vyombo vya habari, umma unaweza kupata taarifa muhimu kwa haraka na kwa wakati, ikiwemo namna ambavyo wananchi wanaweza kutumia mabadiliko na ukuaji wa teknolojia, kurasimisha biashara kupitia kwa Wakala wa usajili wa biashara na leseni (BRELA).
“Niwaombe ndugu zangu wanahabari, kupitia kalamu zenu na vipaza sauti mtusaidie katika kuhakikisha taarifa za BRELA zinatiliwa mkazo ili kuwezesha umma wa Watanzania kwa ujumla kuhamasika katika kurasimisha biashara zao ukizingatia urasimishaji wa biashara hizo zinafanyika kwa njia ya mtandao,” amesema.
Ameongeza kuwa: “Natambua ukuaji wa teknolojia huweza kuwa kikwazo lakini hatuwezi kusimama wakati dunia inakimbia kutokana na mabadiliko na ukuaji wa teknolojia. Hivyo, changamoto kama hizi ninyi waandishi ndipo taaluma yenu inapohitajika katika kuwaelimisha na kuwaongoza.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, amesema mafunzo hayo yanahusisha waandishi wa habari za magazeti, televisheni, radio na mitandao ya kijamii.
Nyaisa amesema uekelezaji na ufanikishaji wa majukumu ya BRELA yanaongozwa na mpango wa miaka mitano wa taasisi kuanzia 2021/2022 hadi 2025/2026, ambao pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha taasisi inaweza kutoa huduma bora na kuwajengea ufahamu kuhusu majukumu yake na namna ya kutumia mifumo yake.
Amesema BRELA itaanza kutoa tuzo maalum kwa waandishi wa habari za biashara ambao watakuwa wakiandika makala zenye matokeo chanya kwa jamii.
BRELA ni wakala wa serikali inayosajili makampuni, majina ya biashara, alama za biashara na huduma, kutoa hataza, leseni za biashara kundi A na Leseni za viwanda.
Kauli mbiu ya mafunzo hayo ya siku nne ni ‘Vyombo vya habari ni chachu ya ukuzaji biashara.’
Trending
- BRELA, UDSM wawanoa wadau faida miliki ubunifu
- Utafiti kilimo, mifugo na uvuvi kutokomeza njaa
- NMB yaja na mwarobaini mikopo kausha damu
- TARI kuzalisha miche 100,000 ya parachichi msimu ujao
- BBT YAANZA KUZAA MATUNDA KWENYE UVUVI
- MAREKANI YATOA BIL 60/- KUIMARISHA USALAMA WA CHAKULA
- BOT YAONYA APP ZA MIKOPO MTANDAONI, YAPIGA MARUFUKU UDHALILISHAJI
- VIJANA, WANAWAKE WAPEWA MITAJI WEZESHI MILIONI 101/-