Na Restuta James
MKOA wa Kagera unatarajiwa kuunganishwa kwenye gridi ya taifa baada ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kusaini mkataba wa kusimamia ujenzi wa vituo vya kupoza na kusafirisha umeme wa kilovoti 220.
Mradi huo utagharimu dola za Marekani milioni 135.4 na utasimamiwa na kampuni ya Shaker Consultancy ya Misri ambayo ni mhandisi mshauri kwa kushirikiana na kampuni ya usimamizi wa miradi ya umeme ya Saudi Arabia (PDC).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 13, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa kusaini mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Gissima Nyamo-hanga, amesema mradi huo utahusisha ujenzi wa kituo cha kupooza umeme wa msongo wa kilovoti 220 hadi kilovoti 30, kitakachojengwa wilayani Ngara.
“Ujenzi wake utahusisha ufungaji wa mashine umba mbili, kazi ya pili itakuwa ni kandarasi ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 220 yenye urefu wa kilometa 166.17 kutoka Benaco (Ngara) hadi Kyaka (Misenyi) na tatu ni ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme wa kilovoti 33 takribani kilometa 683 na mashine umba takribani 64 katika vijiji ambako mradi utapita,” amesema.
Amesema mradi utawaunganishia wananchi 3,226 umeme na kwamba lengo ni kuhakikisha wakazi wa vijiji ambavyo mradi unapita wananufaika.
Nyamo-hanga, amesema mradi huo utajengwa kwa miezi 24 kuanzia Januari mwakani na kwamba utaziondoa Wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi, Muleba, Bukoba Vijijini na Manispaa ya Bukoba, kwenye utegemezi wa umeme kutoka Uganda.
Amesema serikali inatumia Sh. bilioni 2.6 kwa mwezi kununua megawati 21 za umeme kutoka Uganda kuhudumia wilaya hizo.
“Tunachokisema hapa ni kwamba umeme unaotumika Kagera tunaununua Uganda, Mradi huu tuliosaini leo ni muhimu kwa mkoa wa Kagera na nchi kwa ujumla,” amefafanua Nyamo-hanga.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Shaker, Dk. Ismail Shaker, ameahidi kusimamia mradi huo kwa ufanisi ili utakapokamilika ukidhi matarajio ya nchi.
Fedha za ujenzi wa mradi huo zinatolewa na Serikali ya Tanzania, (Sh. bilioni 6.2), Mfuko wa maendeleo Saudi (Dola za Marekani milioni 13), Mfuko wa Maendeleo wa Abudhabi (Dola za Marekani milioni 30) na Mfuko wa Maendeleo wa Shirika la wauzaji mafuta duniani (OPEC) utakaotoa dola za Marekani milioni 60.
Mradi utasimamiwa na Shaker Consultancy Group kwa kushirikiana na TANESCO na mkandarasi anatarajiwa kupatikana Desemba mwaka huu.