Na Restuta James
KAMA huna fedha za kutosha na unahitaji jiko la nje wala usiwaze tena. Kuna njia za kuwa na sehemu ya kupikia yenye hadhi nzuri na mandhari ya kuvutia na kuifanya nyumba yako kuwa ya kisasa kila wakati.
Mtaalamu wa bustani, Georgia Lindsay, ameandika kwenye mtandao wa Houzz kuwa jiko la nje linaweza kuwekwa kwenye eneo la bustani kwa kuweka karo la kuoshea vyombo, vyakula na jiko lenyewe. Hii ni aina ya ubunifu ambao unawapa nafasi wenye nyumba kufurahia mazingira ya nje badala ya kila siku kutumia ndani pekee.
Katika eneo hili la jiko, wanafamilia wanaweza kufurahia mlo hapo hapo nje kwa kuandaa mazingira yaani kuweka meza na viti au mkeka kwa wanaopenda kukaa chini.
Mtaalamu mwingine wa bustani, Anna Elias, anasema jiko la aina hiyo linaweza kuongezewa thamani kwa kuweka ‘vibenchi’ vya watoto ambavyo wanaweza kuvitumia kuchora na kupaka rangi aina mbalimbali ya kazi wanazoandaa.
“Jiko hili linapendeza kama kutakuwa na maua au miti ili kuondoa hali ya jiko la ndani. Pia unaweza kuezeka ili uweze kulitumia wakati wa mvua au jua kali. Ni zuri sana pale ambapo unaalika marafiki au ndugu kwa chakula cha mchana au usiku,” anasema.
Anna anasema jiko hilo linawawezesha wageni na wenyeji kufurahia mlo kwa kuona jinsi unavyoandaliwa na pengine watu wanaweza kuonja wakati wa kupika hadi chakula kinaiva.
“Katika jiko hili mnaweza kujikuta familia nzima mnapika, ni eneo zuri sana,” anasema.