Na Mwandishi Wetu
MILANGO imefunguliwa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kunufaika na mafunzo ya umahiri katika nchi za Ulaya na Marekani, kupitia programu ya kimataifa ya mafunzo kazini.
Aidha, wanafunzi waliopo katika vyuo vya kati vinavyotoa stashahada (diploma), ya kilimo na mifugo wanapewa nafasi hiyo, inayotolewa na Chama cha Ushirika cha Wajasiriamali Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUGECO).
Akizungumza kwenye mjadala wa Jiajiri uliofayika SUA, Mkurugenzi Mkuu wa SUGECO, Revocatus Kimario, amesema fursa hiyo inawahusu wanafunzi kuanzia mwaka wa pili wanaosoma kozi za sayansi ya mifugo, ranchi, dawa za mifugo, ufugaji, afya ya mifugo na kilimo kwa ujumla.
Kozi nyingine ni utalii, usimamizi wa hoteli, sayansi ya chakula na teknolojia, uhandisi mitambo, sanaa ya upishi, agronomia, kilimo cha bustani, sayansi ya mazao, sheria, usimamizi wa biashara, elimu katika sayansi, sayansi ya mazingira na uhandisi wa ujenzi.
Amesema fursa hiyo ni kwa wanachuo ambao wanaendelea na masomo na kwa wahitimu wa kozi hizo kutoka vyuo vinavyotambulika na serikali ambao watapelekwa katika nchi za Denmark, Ujerumani, Sweden, Uholanzi, Israel, Norway na Marekani kwa miezi 18.
“Lengo letu ni kuhakikisha vijana wanapata ujuzi wa kutosha na kuwajengea uwezo zaidi kwenye kile walichojifunza ili kwanza waisaidie nchi na pia wawe na sifa ya kufanyakazi popote duniani. Tunataka tuboreshe kilimo nchini kiwe cha kibunifu na cha kibiashara, tuzalishe kwa tija ili tusaidie uchumi na maendeleo ya nchi yetu,” amesema Kimario.
Kimario alisema walianza kwa kupeleka wanafunzi 20 nchini Israel mwaka 2015 na sasa wanaweza kupeleka zaidi ya wanafunzi 3,500 katika nchi ambazo wameingia nazo makubaliano.
Amesema hivi sasa kuna vijana 500 wanapata mafunzo hayo nchini Marekani na 600 katika nchi za Denmark, Ujerumani, Norway, Uholanzi, Israel na Sweden na kwamba baadhi ya vyuo vimekubali kuyatambua na kutoa alama kwenye vyeti vyao.
“Kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa fani yoyote wanafursa ya kupata haya mafunzo kwa miezi mitatu nchini Ujerumani, wanaenda Juni hadi Oktoba kila mwaka. Kigezo kikuu ni lazima awe mwanachuo,” amesema.
Kimario amesema programu nyingine waliyonayo ni ya kuatamia mawazo bunifu ya biashara na tafiti, ili kuchochea ukuaji wa kilimo na biashara kwa lengo la kuzalisha ajira za kutosha.
Alisema: “Kazi kubwa inayofanywa na SUGECO ni kubadilisha mtazamo wa vijana kuhusu kilimo kwa kutambua kuwa bidhaa za kilimo ndizo biashara kubwa zaidi duniani.”
Aidha, amesema changamoto ya fedha kwa ajili ya maandalizi muhimu ya awali kwa wanafunzi wanaopata nafasi hizo yametatuliwa na benki ya CRDB ambayo imetenga EURO milioni 24 (takribani Sh. bilioni 67); ili kuyafanikisha pamoja na mtaji anzia wanaporejea nchini.
Katika hatua nyingine, Kimario amesema kwa wahitimu wa fani za mifugo, ufugaji wa nguruwe, kuku, farasi, kilimo cha bustani na maziwa, wana nafasi ya kuongeza ujuzi kupitia programu ya kwenda kufanyakazi kwa muda mfupi nchini Norway.
Mwenyekiti wa bodi ya SUGECO na mwanzishi wa ushirika huo, Dk. Anna Temu, amesema ilianzishwa mwaka 2011 ili kuwezesha tafiti na wanasayansi wanaohitimu katika vyuo vikuu, wanatumika kuimarisha uchumi na maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa operesheni na ubunifu wa SUGECO, Joseph Massimba, amesema dunia inataka ubunifu wa hali ya juu na mtaalamu mwenye upekee anayeweza kufanyakazi bila kusukumwa.
“Chochote unachosomea, haya dunia inayoyataka hutoyakwepa…ubunifu, ubobevu kwenye fani yako na umahiri wa ufanyaji kazi. Fursa zilizopo kwenye programu hizi zinakupa nafasi ya kujiimarisha kwenye uwezo, mazingira mapya, teknolojia na tamaduni mbalimbali,” amesema.
“Tunataka tukikushusha Afghanistan, Israel, Kenya, Botswana na kwingineko ufanyekazi inayohitajika…baadhi ya nchi jirani zinapeleka hadi vijana 200,000 kupitia programu kama hizi; jambo linalowajengea umahiri wa kuwa wataalamu wa kimataifa. Sisi bado tuko nyuma na ndio maana tumefungua wigo wa kozi ili vijana wengi zaidi waweze kwenda,” amesema Massimba.
Amesema serikali imeingia makubaliano ya fursa za kazi na mataifa zaidi ya 10 duniani yanayotoa wigo kwa Watanzania kuajiriwa na kampuni na mashirika ya nchi husika.
Kwa mujibu wa Kimario, SUGECO ina ofisi nne za kanda katika mikoa ya Arusha (Tengeru), Mbeya (Uyole), Pwani (Rufiji) na makao makuu yaliyopo SUA Morogoro na kwamba wanao wawakilishi mikoa ya Kigoma na Singida.