Na Restuta James
CHUO cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, kimeanzisha utafiti kwa ajili ya kutambua mchango wa wanawake mashujaa wa Tanzania walioshiriki harakati mbalimbali za kuijenga nchi kuanzia za kupinga ukoloni na kudai uhuru.
Akizungumza na jijini Dar es Salaam na BUSTANI, Mkuu wa Idara ya Stadi za Jinsia katika chuoni hapo, Dk. Sarah Mwakyambiki, amesema utafiti huo ulianza miaka minne iliyopita na tayari wamewatambua wanawake 63, ambao mchango wao katika harakati za ujenzi wa taifa haujatambuliwa ipasavyo.
“Shujaa kwa mantiki ya ni mwanamke wa kwanza kufanya jambo fulani nchini; tumewatazama ambao kwa kiasi kikubwa walifanyakazi na Mwalimu Nyerere. Utafiti ulianza kutazama wanawake hao kuanzia mwaka 1965 hadi 2020,” amesema.
Amesema kati ya wanawake 63 waliowapata, 59 ndio historia zao zimekamilika na wanne bado hazijakamilika.
Dk. Mwakyambiki, amesema yupo aliyeshiriki vita vya Majimaji, ambaye alikuwa mwanamke pekee aliyenyongwa usiku mweusi, kutokana na kwamba alikuwa mstari wa mbele kutoa taarifa za kinachoendelea kwenye ngome ya wakoloni.
Amesema mwanamke mwingine ni rubani na injinia wa ndege ambaye amekuwa akihudumia na kutengeneza ndege ya rais na za viongozi wakuu wa nchi wanaotembelea Tanzania.
Mwanamke mwingine kwa mujibu wa utafiti huo ni aliyehamasisha harakati za siasa na kupanda mizizi ya CCM hadi ngazi ya shina na ndiye aliyekuwa anazungumza kabla Mwalimu Nyerere hajahutubia kwenye mikutano mingi.
Mwanamke mwingine ni hakimu wa kwanza na mwingine ni aliyefanikiwa kusimamia hoja ya kuondoa kodi ya kiti.
“Kuna mama ambaye alitoa jengo lake kuipa CCM ambalo limekuwa ndizo ofisi za chama miaka mingi iliyopita, wapo wasanii na wataalamu wa ustawi wa jamii,” amsema Dk. Sarah.
Dk. Sarah amesema miongoni mwa wanawake hao, yupo pia ambaye alikuwa Mwafrika na Mtanzania wa kwanza kufanyakazi katika Ikulu ya Tanzania.
“Tunaona sasa hivi mtu anaweza akatoa akafanya jambo kwa kuwa kuna vyombo vya habari na mitandao akaonekana yeye ni wa kwanza wakati kuna watu wamewahi kufanya huko nyuma lakini rekodi zao hazizungumzwi popote. Pia tumefanya kama ni utafiti wa kutoa hamasa kwa wanafunzi wa ngazi ya chini ili waone kuna watu walifanya vitu ambavyo viliwafikisha mbali,” alisema Dk. Sarah.
Katika utafiti huo, watafiti wamepitia nyaraka na magazeti kuanzia ya mwaka 1965 na kufanya mazungumzo na ndugu au wahusika waliopo hai ili kuweka kumbukumbu za utumishi na utendaji wao vizuri.
Utafiti umewaweka wanawake hao katika makundi 12, likiwamo la harakati za kupinga ukoloni, kudai uhuru, elimu, uongozi kitaifa, kimataifa, utumishi wa umma, majeshi, sekta binafsi na michango katika jamii na tayari umekamilika ukisubiri fedha ili uweze kuchapishwa.
SUZAN MASHIBE
Huyu ni rubani na mhandisi wa ndege Afrika Mashariki ambaye alikuwa ni mwanamke wa kwanza aliyepata cheti cha uhandisi wa ndege mwaka 2003 ambaye pia ndiye wa kwanza kupata cheti cha rubani cha FAA na mhandishi matengenezo ya ndege.
Mwaka 2009 Suzan ambaye yuko sekta ya usafiri wa anga, alitunukiwa tuzo ya Askofu Desmond Tutu na tuzo ya mwanamke mjasiriamali mwenye mafanikio.
Anamiliki kampuni ya VIA Aviation inayoshughulikia masuala ya kiufundi katika ndege binafsi, za biashara na za viongozi wa nchi pamoja na wanadiplomasia.
Mwaka 2011 alichaguliwa na Taasisi ya World Economic Forum kuingia katika kundi dogo la vijana wenye vipaji kwenye uongozi wa vijana duniani (Young Global Leader -YGL).