Na Restuta James
NI simulizi ya kusisimia ya msichana mwenye miaka 28, ambaye ni yatima asiyewafahamu baba na mama yake mzazi, aliyepewa msaada wa cherehani na Rais Samia Suluhu Hassan, hivi karibuni.
Si mwingine bali ni Beatrice Mwalingo, ambaye ujumbe wake wa maneno 10 umefanikisha kumtambulisha kwa Mkuu wa Nchi, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwenye dunia ya ushonaji, wateja na kuongeza ajira kwa vijana.
Historia ya msichana huyo imebebwa kwa kiasi kikubwa na mageuzi ya teknolojia kuanzia kujifunza kwake kushona hadi kukutana na msaada wa Rais Samia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Beatrice anasema baba yake alikuwa ni Msafwa wa Mbeya akifanya biashara mpaka wa Tunduma na mama yake alikuwa askari polisi, mpakani hapo wakati wanakutana.
“Sina baba wala mama, nimelelewa na babu na bibi yangu mzaa mama. Bibi alishafariki, babu ndiye yupo na mimi ninamlea. Babu yupo Kigoma. Baba yangu simfahamu maana alifariki nikiwa bado mdogo, na mama alifariki nikiwa na miaka minne,” anasimulia Beatrice.
Anasema kutokana na kuwepo kwa picha za mama yake, kuna mpa picha fulani za maisha ya utoto akiwa naye lakini sio kumbukumbu kamili.
“Mama alikuwa ni mtu wa kushinda kazini, naweza nikasema kupitia picha kumbukumbu inakuja,” anasema Beatrice.
HISTORIA YA USHONAJI
Kwa mujibu wa Beatrice, mitandao ya kijamii imebeba historia ya pekee katika kazi anayoifanya kwani alijifunza kushona kupitia mtandao wa Youtube.
“Nimejifunza kushona kupitia youtube nikiwa Japan mwaka 2019. Nilinunua kicherehani kidogo nikawa nafanya mazoezi mpaka nilipoweza na kuamua kununua cherehani kubwa ambayo nilianza kuwashonea rafiki zangu,” anasema.
Bila kueleza kwa undani, anasema alikwenda Japan akiishi na mpenzi wake aliyekuwa nchini humo.
Anasema kwa mwaka mmoja alifanya mazoezi kwa vitendo akiangalia youtube huku akijishonea nguo yeye na rafiki zake.
“Nina miaka mitano sasa tangu nianze kushonea rafiki zangu na baadhi ya wateja nikiwa kule kule Japan…niliona naweza kufanya kitu kingine zaidi, nikapata wazo kwamba nikija Tanzania naweza kuajiri mafundi ili nishone kwa wingi zaidi, ndipo mwaka jana nikafungua hii ofisi,” anasema Beatrice.
Anasema ofisi hiyo ambayo ipo eneo la Mbomba Mbili, Kivule-Ilala, aliifungua Novemba mwaka jana, akiwa na mafundi 12 ambao watano walienda kula sikukuu Desemba mwaka jana na hawajarejea.
Kuhusu kumtumia Rais ujumbe, anasema hakutarajia kujibiwa. “Unajua watu wakiangalia page (ukurasa) ya Rais kila mmoja ana kitu chake cha kuandika…sasa sijui mimi ni kwa vile nimezungukwa na cherehani kila siku ndilo wazo lililokuja la kuomba cherehani, lakini sikutarajia kama itakuja wala kwamba ataiona na kunijibu.”
Akizungumzia ndoto aliyonayo kwenye biashara yake, Beatrice ambaye anamtunza pia babu yake aliyemlea, alisema anaiona mbali na kwamba hata alipofika, hakufikiria.
Mbali ya kushona, msichana huyo anafuga kuku na bata kwa ajili ya biashara.
Beatrice ambaye bado hajaolewa wala hana mtoto, anasema mwaka jana alianza na kuku 500 ambao amewauza na sasa wamebakia chini ya 40.
Anasema anafuga pia bata bukini na mbwa wasio wa ulinzi.
Anasema mbali ya kushona nguo za wateja wanaofika ofisini kwake, anashona pia nguo za harusi, mabegi ya safari, pochi na nguo za kike na za kiume anazouza kwenye maduka.
Anatoa rai kwa vijana na wanawake kutumia mitandao ya kijamii kujielimisha na pia wasikate tamaa katika kazi wanazofanya.
“Hata kama anapenda kupika, kushona au chochote kile, inabidi afanye mazoezi zaidi ili aendelee kupata uzoefu kuliko kusubiri hadi uwe umekamilika,” anasema.
UJUMBE WA MANENO 10 KWA RAIS
Ujumbe wa Beatrice kwenye ukurasa wa Rais Samia ulisomeka: ‘Ukiwa unarudi nyumbani naomba uniletee zawadi ya cherehani’ ambao ulijibiwa na Rais: ‘Hujambo Beatrice, nimepata wasaa wa kuusoma ujumbe wako. Hongera kwa kazi na kujituma. Wasaidizi wangu watawasiliana na wewe kukusaidia upate mashine uliyoomba kwa shughuli zako. Nakutakia kila la kheri.’
SIKU YA MAKABIDHIANO
Akizungumz ana waandishi wa habari juzi baada ya kukabidhiwa cherehani nne kutoka kwa Rais Samia, Beatrice alisema zitamwongezea nguvu na ajira kwa vijana wanne.
Beatrice alikabidhiwa cherehani nne ambazo ni mbili za kushona kawaida na mbili za kudarizi na hivyo kufanya awe na jumla ya vyerehani 14.
“Nimefurahi kwa sababu ni kitu ambacho sikukitarajia kwamba itakuja iwe ni kitu kikubwa zaidi na nilichokuwa nategemea. Mimi nilivyoomba nilidhani nitapata moja, lakini namshukuru Mungu ameniagizia zaidi ya kile nilichoomba au nilichotarajia,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Hii inaniongezea nguvu ya kuendelea kujituma zaidi na imenivusha kutoka hatua moja kwenda nyingine na kwa hili itawasaidia wenzangu zaidi. Kwa cherehani za kudarizi itanisaidia kwa sababu nitafanyia hapa hapa tofauti na mwanzo nilikuwa naenda kwa wenye nazo. Itakuwa ni urahisi wa kufanyakazi zaidi. Cherehani hizi zitaongeza ajira nne.”
Alisema alianza kwa kununua cherehani tano za mtumba na tano mpya.
“Nilivyopata meseji yake (Rais Samia), kwamba nitapata nilichokiomba imenifungulia milango mingine zaidi…amenitambulisha kwa vijana wenzangu, wateja na kwa watu wengi sana, niseme tu ahsante sana kwake…najiona mwenye bahati,” alisema.
Alisema amepata wateja wengi na amefanikiwa kukutana na makundi mbalimbali vikiwamo vyombo vya habari.
“Natamani sana nimshonee nguo Mheshimiwa Rais na kama nitapata nafasi nimpime mwenyewe nimtengenezee nguo ila kwa leo nampa kuku watano kama zawadi kwakuwa nafuga pia,” alisema.
Alitoa rai kwa vijana kutoitumia mitandao ya kijamii vibaya.
“Tusitumie mitandao kama sehemu ya kupunguzia hasira. Iwe ni sehemu ya kueleza changamoto au mahitaji yetu. Anaweza asikione mhusika wakapita watu wengine wakaguswa na wakakusaidia.