WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la saba la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi ambalo litafanyika Jijini Dodoma Septemba 29, mwaka huu, likiwa na kaulimbiu ya ‘Uwezeshaji wa Uchumi Endelevu’.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa, amewaambia waandishi wa habari Jijini hapa jana kuwa kongamano hilo litatanguliwa na wiki ya uwezeshaji sambamba na maonesho ya siku tatu ya wajasiriamali yatakayoanza tarehe 26 hadi 28, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete.
“Maenesho hayo ya siku tatu kabla ya kongamano yana maana kubwa katika dhana nzima ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwani wajasiriamali watapata fursa ya kipekee kuonyesha biashara zao kwa Watanzania na jinsi wanavyopata mafanikio kupitia uwezeshaji,” amesema.
Amefafanua kuwa: “Kongamano litatoa fursa ya kutathmini utekelezaji wa sera ya uwezeshaji pamoja na taarifa mbalimbali ya utekelezaji wa mambo yaliyokuwa kwenye kongamano la sita ambapo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaagiza wakuu wa mikoa yote kuanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi.”
Mkurugenzi huyo amesema kuwa wakati wa kongamano, tuzo zitatolewa kwa wote waliofanya vizuri ikiwamo Mikoa, wajasiriamali na taasisi mbalimbali.
“Tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo na ufuatiliaji wake wa kutaka kuona kuwa Watanzania wengi na hasa wanawake na vijana wananufaika zaidi na uwezeshaji,” amesema.
Kwa mujibu wa Bi. Issa, kongamano litahusisha Wizara, Mashirika, Wakala na Taasisi za Serikali, Taasisi Binafsi chini ya mwamvuli wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Mikoa, Halmashauri, Wajasiriamali, Taasisi za Fedha, Taasisi za Elimu, Tafiti, Wawekezaji pamoja na wadau wengine wa masuala ya uwezeshaji.
“Wananchi wote wanakaribishwa kujionea na kujifunza masuala mazima ya uwezeshaji, upatikanaji wa mitaji, fursa zilizopo kwenye miradi ya mkakati, masoko na hata kutengeneza mtandao wa watu, Taasisi au Kampuni ya kujiendeleza kiuchumi,” amefafanua Bi. Issa.