MOJA kati ya malengo ya endelevu ya dunia ni kuhakikisha kwamba hadi kufikia mwaka 2033, asilimia 80 ya kaya ziwe zinatumia nishati safi ya kupikia.
Lengo hili linakuja na mageuzi ya kiteknolojia ya uvumbuzi wa majiko yanayotumia nishati kidogo kwa ajili ya kupikia na kuhakikisha upatikanaji wake kwa gharama nafuu ili watu wa kada zote mijini na vijijini, waweze kuzipata.
Majiko yanayotajwa hapa ni yale yanayotumia kuni, mkaa, mafuta ya kupikia (bioethanol), gesi na umeme kidogo. Kutokana na umuhimu wa nishati hasa kwa ajili ya kupikia, Umoja wa Ulaya (EU), nchini umetenga EURO milioni 17 (takribani Sh. bilioni 47.6), kwa ajili ya kuzisaidia kampuni zinazojishughulisha na uzalishaji na usambazaji wa nishati pamoja na majiko hayo ya kisasa, kwa lengo la kufanikisha malengo ya dunia katika kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira.
Mtaalamu wa masuala ya Fedha wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji ya Maendeleo (UNCDF), linalosimamia utekelezaji wa Mradi wa Cookfund, Imanuel Muro, anasema mageuzi ya kiteknolojia ni muhimu ili kupunguza matumizi ya nishati zote za kupikia.
Anasema kupunguza matumizi kutawezekana kwa kuruhusu uvumbuzi wa majiko yanayotumia kiasi kidogo cha nishati, bila kuathiri upishi ili kaya nyingi ziweze kuona umuhimu wa kutumia teknolojia mpya.
Muro ambaye pia ni meneja mradi wa Cookfund, anasema tayari wabunifu wameleta mageuzi ya kiteknolojia katika eneo hilo kwa kuvumbua mkaa na kuni mbadala, majiko ya gesi yanayotumia kiasi kidogo cha nishati hiyo, mafuta (bioethanol) kwa ajili ya kupikia na jiko la umeme linalotumia umeme kidogo.
Anasema katika hilo, kuna mkaa na kuni rafiki wa mazingira (green charcoal), ambao unatokana na majani (nyasi), pamoja na miti inayoweza kukuzwa kwa kipindi kifupi, ambao ukipatikana kwa wingi utapunguza ukataji wa miti ya asili kwa ajili ya mkaa na kuni.
Anasema uvumbuzi mwingine umeleta majiko yanayotumia kuni na mkaa kidogo.
“Unaweza kuona kwamba pamoja na kuwa na mkaa rafiki wa mazingira, teknolojia imetuletea majiko yanayotumia nishati hii kwa kiasi kidogo sana. Majiko haya yanapunguza matumizi ya mkaa kwa asilimia 60 na yamethibitishwa,” anasema Muro.
Muro anasema pia kuna jiko linalotumia gesi kidogo, umeme kidogo na mafuta maalumu ya kupikia (bioethanol), kidogo ambayo yakipatikana kwa wingi yatasaidia kukabili athari za uharibifu wa mazingira.
“Tunachopaswa kufanya ni kubadilisha mitazamo yetu na kutumia nishati hizi rafiki, ili tuweze kuokoa mazingira yetu na hili ndilo suluhisho,” anasema.
Ili kuweza kubadili mtazamo, UNCDF imezindua kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ya ‘Anzia Jikoni-mabadiliko ya hewa safi ya baadae yanaanzia jikoni.’
Anasema kupitia kampeni hiyo, mradi wa Cookfund unalenga kufadhili kampuni na wajasiriamali wanaojihusisha na uzalishaji na usambazaji wa nishati safi.
“Huwezi kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa bila kuleta mabadiliko ya nishati ya kupikia. Ufadhili wa EU unalenga ubunifu wa teknolojia ya kisasa ya kupata majiko yanayotumia mkaa, gesi na kuni kidogo. Tunatoa ruzuku kwa kampuni ili mtumiaji wa mwisho aweze kupata nishati na jiko kwa bei ndogo,” anasema.
Muro anasema kampeni ya ‘Anzia Jikoni’ inalenga kuueleza umma umuhimu wa matumizi ya teknolojia za kupikia zinazopunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Anatoa mfano kwamba kwa kaya zinazotumia kuni kwa ajili ya kupikia, mageuzi ya teknolojia yanaziwezesha kuendelea kutumia nishati hiyo kwa kiasi kidogo, wakiwa na jiko sanifu badala ya kutumia mafiga yanayohitaji kuni nyingi na kupoteza pia moto.
“Huwezi kumwambia mtu ambaye yuko kijijini anayepata kuni za bure atumie umeme au anunue gesi akakuelewa. Jiko sanifu linaweza kumshawishi kwa sababu linamsaidia kupunguza matumizi ya kuni na wakati huo huo, chakula chake kinaiva kwa wakati,” anasema.
Muro anaongeza: “Ufadhili wa EU unalenga kuongeza utaalamu wa kifedha katika uwekezaji ili kuchochea uwezo wa makampuni katika kuvumbua teknolojia safi za kupikia.”
Anasema mradi unalenga kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa za kupikia kwa kuhakikisha upatikanaji wake kwa urahisi.
Maelezo ya Muro yanaungwa mkono na Mratibu wa Kitaifa wa Mradi ya Nishati na Mazingira wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO), Victor Akim, ambaye anasema matumizi ya nishati yanaendea sambamba na majiko yanayotumia nishati kidogo.
“Tunahimiza matumizi ya majiko yanayopunguza matumizi ya nishati ili kila kaya ipate unafuu. Hili litasaidia kukabili athari za kimazingira,” anasema.
Anasema UNIDO inafadhili viwanda vinavyozalisha majiko na nishati mbadala ya kupikia, ili kuwezesha upatikanaji wake kwa wingi.
Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa mradi wa Cookfund, Elizabeth Ngoye, anasema ndani ya miezi mitatu, watumiaji wapya 3,373 wamefikiwa na nishati safi ya kupikia, katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma na Mwanza, inayohusika kwenye mradi huo.
Anasema lengo la mradi huo ni kufikia kaya mpya 580,000 na kuzalisha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, kupitia kampuni 295 zinazokusudiwa kufadhiliwa kifedha na kiufundi.
“Tunategemea kupunguza matumizi ya mkaa zaidi ya tani 185,000 na kuokoa hekari 23,000 za msitu,” anasema.
Mvumbuzi wa jiko linalotumia umeme kidogo, Shukuru Meena, anasema jiko hilo sanifu linapika kwa kutumia presha ya mvuke unaokusanywa ndani ya sufuria.
“Linatumia nishati kidogo kuivisha chakula kwa muda mfupi na kuhifadhi virutubisho hivyo kuokoa muda, fedha, afya na mazingira; unaweza kuivisha maharage kwa umeme wa Sh. 200,” anasema Meena.
Anasema jiko hilo ambalo linamuundo kama lile la kupikia wali, linauwezo wa kupika vyakula vya aina mbalimbali kama maharage, ndizi, kande, mchemsho, ugali na pilau kwa njia ya kuchemsha, kurosti (kuunga), kwa mvuke (steam cooking), kukaanga (frying) na kuoka.