KIOO ni moja ya pambo la ndani lenye ‘ladha’ ya kipekee kutokana na nguvu yake ya kubadili mwonekano wa chumba au eneo kwa ujumla.
Wataalamu wa mapambo ya ndani wanaeleza kuwa kioo ni pambo ambalo limetumika kwa karne kadhaa bila kuchuja thamani yake.
Moja ya sifa ya kipekee ya kutumia kioo kama pambo ni uwezo wake wa kubadili mwonekano wa chumba kidogo kuwa kikubwa na kupunguza eneo kubwa kuwa la kawaida, kulingana na namna ya uwekaji.
Akizungumza na GND mapema leo Juni 9, 2023, mtaalamu wa mapambo ya ndani, Winnie Joseph, anasema kioo ni pambo linalowekwa sehemu tofauti tofauti kuanzia jikoni, sehemu ya kulia chakula, chumbani, koridoni, eneo la kuswakia, bafuni au sehemu aipendayo mwenye nyumba.
Anasema pamoja na kwamba kioo kimezoeleka, iko njia ya kufurahia pambo hili la karne kutokana na wataalamu kubadili mwonekano na ubora wake.
Winnie anasema hivi sasa kioo kimekuja na taa mahsusi huku kikiwa na teknolojia ya kuondoa ukungu kwa wale waliokiweka bafuni na kuoga kwa maji moto.
“Siyo tu hivyo, design (aina) mpya ya hili pambo imekuja na sehemu ambayo unaweza kuunganisha simu yako kupitia bluetooth na kusikiliza muziki unaoupenda huku ukioga au kujipaka mafuta,” anasema.
Anasema vioo vilivyoboreshwa kwa uwezo huo ni vikubwa akigusia pia pambo la vioo vidogo, ambavyo vikiwekwa vingi sehemu moja vinavyoongeza mwonekano.