SEHEMU ya kulia chakula ni moja ya eneo muhimu ndani ya nyumba yoyote na ndio maana mtu anapojenga nyumba anazingatia eneo hili.
Mtaalamu wa mapambo ya ndani, Simon Alex, anaeleza kuwa mabadiliko makubwa yanayoendelea kwenye sekta nyingine yameigusa pia sekta ya nyumba na mazingira kwa ujumla, akizungumzia eneo la chakula.
Akizungumza GND anasema chakula hakipaswi kuwekwa kwenye meza ya chakula watu wanapokaa na kula.
Badala yake, anasema meza ya bufee ndio inayopaswa kuwekwa chakula na inatakiwa iwekwe pembezoni mwa meza ya chakula ili iwe rahisi kwa mtu anapopakua chakula kufika mezani kula.
Anasema meza hiyo inapaswa kuwa ndefu kiasi na sharti iwe na kioo kikubwa ili mtu anayepakua chakula aweze ‘kutupia’ jicho kujitazama.
Meza hii inaweza kuwekwa mshumaa, ua na glasi nzuri za maji, juisi na matunda, ili mtu anayesubiria chakula aweze kujipooza na kinywaji au tunda alipendalo.
Kwa mujibu wa Simon, mbali ya kuweka chakula, meza ya bufee ni ‘pambo’ nzuri ndani ya nyumba kwani inaongeza unadhifu na ‘kupunguza’ vyombo kwenye meza ya kulia chakula.