MAMLAKA ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA), imeita wawekezaji wenye nia ya kuanzisha viwanda ili waendeleze maeneo saba yaliyopo katika mikoa ya Mbeya, Lindi, Dar es Salaam, Tanga na Shinyanga, chini ya utaratibu wa mamlaka hiyo.
Taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Charles Itembe, kwa vyombo vya habari imeyataja maeneo yaliyopo Dar es Salaam kuwa ni vitalu namba 184/185 na 186/185 vyenye jumla ya ekari 8.39, zilizopo eneo la viwanda Chang’ombe, katika Manispaa ya Temeke, zilizokuwa zinamilikiwa na iliyokuwa kampuni ya taifa ya chuma.
Lingine kwa Dar es Salaam ni mita za mraba 15,000 zilizopo eneo Maalum la Kiuchumi la Benjamin William Mkapa, Mabibo External, ambalo ni maalumu kwa shughuli za kibiashara.
Mkoani Tanga, EPZA imetangaza shamba namba 11 lenye ukubwa wa ekari 36, lililopo Kijiji cha Mkata, kando ya barabara ya Mkata – Handeni, takribani kilomita moja kutoka makutano ya barabara ya Dar es Salaam-Tanga, wilayani Handeni.
Kwa mujibu wa Itembe, mkoani Lindi kuna maeneo mawili ambayo ni ekari 9.97 zilizokuwa za kiwanda cha Korosho Wilaya ya Nachingwea na ekari 9.81 zilizokuwa kiwanda cha kusindika mafuta ya ufuta wilayani humo.
Katika mikoa ya Shinyanga na Mbeya, EPZA imetangaza ekari 1431.62 za maeneo yaliyokuwa yanamilikiwa na kampuni ya Tanganyika Packers.
Mgawanyo wa maeneo hayo ni ekari 1179.23 lililopo Mwalugoye Shinyanga na ekari 252.39 zilizopo barabara ya Chunya, Mbalizi.
“Maeneo yote yanafikika kwa barabara na yana huduma zote muhimu kama umeme na maji,” alisema Itembe katika taarifa hiyo.