SHIRIKA la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Mkoa wa Dar es Salaam, limekuja na mkakati wa kusaidia wajasiriamali wadogo kumiliki viwanda baada ya kujenga kituo cha kisasa cha kusindika mazao ya kilimo, chenye huduma muhimu za viwanda vidogo.
Meneja wa SIDO, Mkoa wa Dar es Salaam, Ridhiwani Matenge, amesema kituo hicho kinajengwa kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Korea (KOIKA) na kipo mbioni kukamilika.
“Ni kituo ambacho kitaweza kutoa mafunzo na uzalishaji kwa wakati mmoja ambapo wajasiriamali watapata mafunzo kwa vitendo na pia itakuwa ni sehemu ya kuzalishia. Jengo hilo likikamilika na kuwekwa vitendea kazi, litakuwa na maeneo sita ya mafunzo na uzalishaji,” amesema.
Amesema watakaonufaika na kituo hicho ni wajasiriamali wenye nia ya kuanzisha viwanda vya kuoka mikate (bakery and confectionaries), usindikaji wa maziwa, utengenezaji wa aina mbalimbali za juisi, mvinyo, viungo vya chakula na uongezaji wa thamani wa asali.
“Watakuwa wanapata mafunzo na uzalishaji na wakati huo huo wanaweza wakaja na malighafi zao wakazalisha, wakafungasha, wakaondoka. Ndiyo faida ya pekee ya mradi huu ambao umekidhi matakwa ya viwango vya mamlaka nyingine kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS),” amesema.
Matange amesema nia ya SIDO ni kuwawezesha wale wenye nia ya kuanzisha viwanda lakini wanakosa majengo, kupata eneo linalokidhi viwango stahiki kwa ajili ya kulinda usalama na ubora wa vyakula.
“Kitakuwa ni kituo cha kisasa na cha mfano kwa mkoa wetu wa Dar es Salaam, kitakuwa na huduma zote yaani mashine zitakazowezesha uzalishaji wa maeneo niliyoyataja,” amesema Matange.
Ameongeza kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ni moja ya soko kubwa la mazao ya kilimo nchini, hivyo kujengwa kwa kituo hicho ni fursa kwa wakazi wa jiji hili kuchangamkia fursa ya kuanzisha viwanda kupitia shirika hilo.
Matange amefafanua kuwa kituo kitaweza kuhudumia wajasiriamali 20 kwa mara moja, kutoka kila kundi la bidhaa zilizotajwa.