Benki ya NBC imetoa gawio la Sh. bilioni sita kwa Serikali, ikiwa ni sehemu ya faida iliyopatikana mwaka 2022.
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya hundi iliyofanyika leo Mei 17, Jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, ameipongeza NBC ambayo Serikali ni mmoja ya wanahisa, ikimiliki asilimia 30 ya hisa zake, amesema mafanikio hayo ni matokeo chanya ya utendaji mzuri uliowezesha kupatikana kwa faida nzuri.
“Serikali inafurahi kuona uwekezaji wake unakuwa wenye tija. Kiasi cha shilingi bilioni sita tulichopokea leo, kitasaidia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo,” amesema Mchechu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NBC, Elirehema Doriye, amesema mafanikio ambayo Benki imepata yamechangiwa na uaminifu ambao wateja wameijenga kwa Benki hiyo.
“Faida yetu kabla ya kodi imekua kwa asilimia 36 kufikia Sh. bilioni 81.9 kutoka Sh. bilioni 60 mwezi Disemba 2021. Faida hii imetuwezesha kutoa gawio la shilingi bilioni 20 kwa wanahisa wetu ikiwamo Serikali ambayo leo tunakabidhi hundi ya shilingi bilioni sita,” amesema Doriye.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, ameishukuru Serikali kwa kutengeneza mazingira rafiki ya biashara ambayo yameiwezesha NBC kukua kila siku.
“Utendaji na faida tuliyopata ni uthibitisho wa mazingira mazuri ya biashara ambayo serikali imeyatengeneza ambayo yametuwezesha kuwafikia wateja wengi zaidi na kutengeneza faida zaidi. Tutaendelea kufanya uwekezaji kwenye upanuzi wa mtandao wetu wa kibenki na kuwekeza zaidi katika teknalojia, ili kukidhi mahitaji ya wateja wetu,” ameeleza Sabi.