DODOMA, Tanzania
WAKATI watu wengi wakitazama njiwa kama kitoweo na mapambo, ndege huyo anaweza kufugwa kibiashara na kuiingizia familia kipato cha kutosha.
Deogratius Temba, kijana kutoka Dodoma, Tanzania anafuga njiwa wa kipekee na wanamuingizia kipato cha kutosha.
Njiwa anaofuga Temba maarufu kama Manjiwa hutumika kupendezesha makazi, maofisi ama sehemu zingine kama mahoteli na za kupumzikia.
Kati zaidi ya aina 10 ya njiwa wa mapambo alionao Deogratius, mmoja anauzwa kati ya dola $85 mpaka $180 au Sh. 400,000.
Unaweza kujiuliza wanafananaje njiwa hawa, na kwanini kijana huyu maarufu kama Deo Manjiwa ameamua kuwafuga njiwa hawa wa mapambo? Mwandishi wetu Yusuph Mazimu alimtembelea huko Dodoma kujua mengi.
HISTORIA YA NJIWA HAWA
Ufugaji wa njia ulianza miaka zaidi ya 5,000 iliyopita. Njiwa walifugwa kienyeji na kawaida. Wafugaji waliwafuga kwa madhumuni tofauti ikiwamo kutumika kama kitoweo, baadhi kuwatumia kupeleka ujumbe (vikaratasi ama kufika kwao), wakifundishwa kwa namna mbalimbali.
Lakini katika kipindi cha miaka 50 iliyopita ufugaji wa njiwa kama ‘hobby’ au kwa kujifurahisha ama kwa kupenda kulianza kushika kasi na sasa karibu kila mahali ufugaji wa kibiashara umeanza kushika kasi.
“Wakati nataka kuanza kuwafuga hawa njiwa majirani hawakuwa na shida ila mke. Shida ilikuwa kwa mke wangu, kwa sababu wakati nataka niwanunue mke wangu aligoma kabisa,” anasema Deo Manjiwa na kuongeza: “Alisema unanunua njiwa Sh. 1,200,000 ni njiwa gani, nikamwambia wewe tulia utawaona,” anasema.
ULAJI WAO
Tofauti kubwa ya njia hawa wa mapambo iko kwenye maeneo manne. Ulaji wao, maisha yao, muonekano wao na kustahili kwao ugumu wa mazingira.
Wana muonekano mzuri wa kupendeza. Muonekano unaobebwa na rangi zao, muundo wa maumbo yao, manyoya yao yaliyokaa na namna wanavyotembea. Na hiki kinawatofautisha na njiwa wengine wa kawaida. Njiwa wa asili.
Hawa hawawezI kuvumilia mazingira magumu. Lakini ukiwaweka kwenye mazingira ya ‘kizungu’, wanaweza kuzaliana sana. Ndani ya mwaka mmoja Deo Manjiwa amefanikiwa kuzalisha mamia ya njiwa kutoka njiwa sita alioanza nao.
Ukiacha magonjwa ya mafua kama wanavyoumwa njiwa wengine, Deo analalamika tu ulaji mkubwa wa njiwa hawa.
“Kwa siku wanaweza kula kilo tano au nne,” anasema.
Ulaji huu unamtisha mmoja wa watu waliokuja kushangaa njiwa hawa nyumbani kwa Deo Manjiwa, eneo la Makole, Dodoma.
NJIWA NI BIASHARA KUBWA
Deo Manjiwa anathibitisha njiwa ni biashara kubwa. Alianza na mtaji wa njiwa sita kutoka Zanzibar. Sasa ana mamia ya njiwa wenye thamani ya zaidi ya milioni 25 sawa na karibu dola za Marekani 10,000.
“Njiwa wote hapa tukiwauza kwa Sh. 200,000 kila mmoja labda tuseme wako njiwa 100. Laki mbili mara mia inakuja milioni 20. Lakini kila 200,000 ukiziweka kwa gharama za mchele wa sasa hivi unapata kilo 66. Na kilo 66 kwa familia ya watu wanne au watano wanaweza wakala kilo 1. Kwa hivyo thamani ya njiwa mmoja ya 200,000 inaweza kulisha familia kwa miezi miwili. Kwa hiyo njiwa sio mapambo tu njiwa pia ni kipato,” anasema.
Lakini kwa bei ya mchele kijijini isiyozidi 2,500 kwa kilo, njiwa anayeuzwa Sh. 400,000 anaweza kukupa zaidi ya kilo 100 za mchele.
WANALIWA?
Kwa mujibu wa Deo Manjiwa, ni njiwa wanaoliwa kama njiwa wengine. Tena kwa sababu ni wakubwa kwa maumbo, wapo wanaofikia maumbo kama kuku wa kawaida, ni wazuri kwa familia.
“Huwa nawachinja sana, hasa wale wenye rangi ambazo naona sokoni hazitavutia au wanaoumwa,” anasema na kueleza kuwa hapendi kufanya hivyo kutokana na kwamba wana thamani kubwa.
“Yaani njiwa wa Sh. 400,000 umchinje tu? anahoji Deo huku akiendelea kuwahudumia njiwa wake kwenye mabanda yake mawili makubwa.
BBC