Mwonekano wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere
Na Restuta James
MIEZI minne baada ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuzindua ujazaji wa maji katika bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere (JNHPP), katika Mto Rufiji, mkoani Pwani, ujenzi wake umebakisha asilimia 14.4 pekee kukamilika.
Bwawa hilo linalotazamiwa kuzalisha megawati 2,115 za umeme litakapokamilika, limebakisha ujazo wa maji futi 10.53 pekee, kuanza uzalishaji wa awali.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewaambia waandishi wa habari leo kwamba ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 85.6.
“Bwawa letu la Mwalimu Nyerere ni moja ya miradi ambayo inakwenda vizuri na utekelezaji unaendelea…mwakani Juni tunataka tuanze kuzalisha umeme kutoka bwawa la Nyerere na wataalamu wanatuambia Januari tunaanza kuuawasha maana kazi ya kujaza bwawa inaenda vizuri,” amesema Msigwa.
Amesema wataalamu wameiambia serikali kwamba ujazo wa maji ukifika futi 163, kutoka usawa wa bahari, uzalishaji unaweza kuanza.
Sambamba na taarifa ya Msigwa, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Maharage Chande, leo Aprili 20, imeeleza kuwa ujazaji wa maji katika bwawa hilo umefikia urefu wa mita 146.53 kutoka usawa wa bahari.
Amesema ujenzi unaendelea vizuri na kwamba mategemeo ni kukamilisha mradi huo kwa muda muafaka kama ilivyopangwa.
“Hadi leo (jana), kina cha maji katika bwawa la JNHPP kimefika urefu wa mita 146.53 toka usawa wa bahari,” amesema.
Rais Samia alizindua rasmi ujazaji wa maji katika bwawa hilo Desemba 22, mwaka jana na kuahidi kuwa serikali yake itaukamilisha kwa wakati mradi huo wa kimkakati.
Mradi huo unatarajiwa kuzalisha megawati 2,115 za umeme utakapokamilika ambao njia yake ya kuchepusha maji ina urefu wa mita 703 na upana ni kipenyo cha mita 12.
Mradi wa JNHPP unaoshika nafasi ya kwanza kwa ukubwa katika miradi yote inayotekelezwa katika nchi za Afrika Mashariki na ni wa nne kwa miradi yote inayotekelezwa Afrika.
Mradi unaoshika nafasi ya kwanza Afrika ni wa Grand Ethiopian Renaissance Dam (6,400 MW) uliopo nchini Ethiopia, namba mbili ni ule wa Batoka George Hydroelectric Dam (2,400 MW), wa nchini Zambia katika Mto Zambezi na wa tatu ni mradi wa Caculo Cabaco Hydroelectric Dam (2,172 Mw) wa nchini Angola.