Na Restuta James
SERIKALI imetangaza neema ya ufadhili wa masomo kwa vijana 8,000, ambao watagharimiwa kwa asilimia 100 kusomea ufundi stadi wa aina mbalimbali.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), juzi ilieleza kuwa ufadhili huo ni ruzuku ambayo walengwa hawatarudisha kama inavyofanyika kwa wanaojiunga vyuo vikuu nchini.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa vijana wanaopaswa kuomba ufadhili huo ni wenye umri wa miaka 15 hadi 35; na yatatolewa chini ya programu ya kukuza ujuzi nchini, inayolenga kuwezesha nguvu kazi ya Taifa kupata ujuzi na stadi za kazi stahiki, ili kumudu ushindani katika soko la ajira. Watengenezaji matofali nao wamekumbukwa.
“Ofisi imeingia makubaliano na vyuo 52 vinavyotoa mafunzo ya ufundi stadi ambavyo vimesajiliwa na Mamlaka husika kutoa mafunzo katika fani mbalimbali zikijumuisha ubunifu wa mitindo na ushonaji nguo, ufundi bomba, uashi, useremala, uchomeleaji na uungaji vyuma,” ilisema taarifa hiyo.
Ilisema fani nyingine ni upakaji rangi na maandishi ya alama, upishi, utengenezaji wa vipuri vya mitambo, ufundi magari na mitambo, umeme wa majumbani na viwandani, umeme wa magari, huduma za hoteli na utalii, ukataji madini na ufundi vyuma.
“Ofisi inapenda kuwatangazia vijana wa Kitanzania wenye umri kati ya miaka 15 hadi 35, wanaopenda kujiunga na mafunzo katika mojawapo ya fani ilizoorodheshwa wafike katika vyuo vya VETA (Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi), vya Mikoa na Wilaya pamoja na vyuo vilivyoainishwa, ili kuchukua fomu ya kuomba kujiunga na mafunzo. Serikali itafadhili ada ya mafunzo kwa asilimia 100,” ilifafanua.
Ilisema mwanafunzi, mzazi au mlezi atagharamia nauli ya kwenda chuoni na kurudi nyumbani, kwa kuwa mafunzo hayo yatakuwa ya kutwa.
“Sifa za kujunga na mafunzo haya ni elimu ya msingi au zaidi kwa fani za ubunifu wa mitindo na ushonaji nguo, ufundi bomba, ujenzi, useremala, uchomeleaji na uungaji vyuma, upakaji rangi na maandishi ya alama,” ilieleza.
Taarifa hiyo ilifafanua kwamba kwa fani ya utengenezaji wa vipuri vya mitambo, ufundi magari, umeme wa majumbani na viwandani, umeme wa magari na umeme wa jua (solar), waombaji wanapaswa kuwa na elimu ya kidato cha nne na kuendelea.
Aidha, ilisema vijana wenye ulemavu watapewa kipaumbele katika nafasi za mafunzo hayo.
Hata hivyo, mbali ya vyuo vya VETA, taarifa hiyo imetaja vyuo vingine vikiwamo vya binafsi vitakavyotoa mafunzo hayo, kwa makubaliano na serikali.
Idadi ya vyuo hivyo kwenye mabano kwa kila Mkoa ni Arusha (2), Dar es Salaam (2), Dodoma (3), Geita (1), Iringa (2), Katavi (1), Kagera (3), Kigoma (2), Kilimanjaro (3), Lindi (2), Manyara (1) na Mara (3).
Mikoa mingine ni Mbeya (4), Mtwara (2), Morogoro (2), Mtwara (2), Pwani (2), Mwanza (3), Rukwa (1), Ruvuma (4), Shinyanga (2), Singida (2), Tabora (3) na Tanga (2).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kuna mafunzo yanayotolewa kwenye mikoa kadhaa, huku mingine ikiwa haiyatoi, ikiwamo huduma za ndani na utunzaji wa vyumba vya wageni, utalii na usafirishaji pamoja na kuongoza watalii.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa kwa Mkoa wa Dar es Salaam, mafunzo yametoa kipaumbele kwenye fani za ufundi magari, useremala, upishi, uchomeleaji na uungaji wa vyuma, uchongaji vipuri, umeme wa majumbani, umeme wa jua, ubunifu na ushonaji wa nguo na ufundi bomba.
Kwa Mkoa wa Dodoma, mafunzo yanafanana na ya Dar es Salaam japokuwa kuna nyongeza ya fani za ufundi wa mitambo, uendeshaji wa mitambo, umeme wa magari, uashi na ufugaji wa wanyama na nyuki.
Jijini Mwanza, mafunzo mahsusi ni upakaji rangi na uandishi wa alama, ukarabati wa mashine za kuchakata pamba na kazi za aluminium wakati Arusha, fani mahsusi ni utalii na usafirishaji.
Kwa mkoa wa Morogoro, pamoja na mafunzo mengine, wanafunzi watafundishwa mapishi na ukarimu, wakati mkoani Mbeya moja ya fani mahsusi ni ufundi viyoyozi na majokofu, marumaru na terazo pamoja na kazi za aluminium na PVC. Ufadhili kuwalenga wanaopenda masuala ya saluni na urembo.