Taasisi za serikali na vyuo vikuu, zimetangaza mkakati wa kuwafaidisha wabunifu na watafiti, kutumia kazi zao kibiashara na kujipatia maendeleo, badala ya kazi zao kuishi kwenye makabati.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. William Anangisye, aliyasema hayo juzi Novemba 04, 2024 jijini Dar es Salaam na kutoa rai kwa wabunifu kuchangamkia utajiri uliopo kwenye miliki ubunifu (IP), alipokuwa akifungua mafunzo ya wataalamu mbalimbali kuhusu eneo hilo.
Alisema uwekezaji na viwanda, vinategemea ubunifu na utafiti ili kuzalisha bidhaa mpya au kuboresha zilizopo na kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
“Watu wanafanya utafiti unaishia kwenye makabati tu, lakini sasa hivi tunataka utafiti na ubunifu wetu uwe bidhaa kwa ajili ya biashara. Sisi kama UDSM tumebobea katika masuala ya miliki ubunifu, tuna ofisi hapa chuoni na tuna shahada ya uzamili ya masuala haya. Hatutaki tafiti ziishie kwenye makabati, tunataka zitumike kuwanufaisha Watanzania wote,” alisema.
Prof. Anangisye alisema mafunzo hayo yanawahusisha watu wa kada mbalimbali wakiwamo majaji wa Mahakama Kuu na mawakili, ili kujenga uwezo wa mamlaka nyingine katika kusimamia miliki ubunifu, kwa lengo la kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini.
“Malengo mawili ya sisi kukutana hapa siku ya leo ni kwa sababu dunia ni kama kijiji na mwingiliano ni mkubwa kati ya nchi na nchi. Kuna mambo mapya yanayokuja na ndio maana kuna haja ya kuwafundisha wenzetu ili waone umuhimu wa kubiasharisha tafiti na bunifu kwa nia ya kuongeza uthamani wa utafiti na ubunifu wa watu wetu,” alisema.
Alisema miliki ubunifu inavutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje, hivyo inaongeza mitaji, kuzalisha ajira na kuleta mageuzi ya kiuchumi.
Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara (Brela), Godfrey Nyaisa, alisema Watanzania wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu miliki ubunifu na kwamba lengo la mafunzo hayo ni kuzalisha wataalamu wengi watakaotoa elimu kwa umma kuhusu fursa zilizopo katika ulinzi wa ubunifu kisheria.
“Wapo wananchi wenye bunifu ambazo hazina sifa, wengine wanazo zinazohitaji kuboreshwa na kuna nyingine zina sifa lakini hawajui waende wapi wakazilinde. Bunifu ni ajira na ni eneo lenye utajiri mkubwa sana,” alisema.
Alisema washiriki wa mafunzo hayo wametoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Malawi, Zambia na Tanzania, yakiwahusisha majaji, mawakili, wataalamu kutoka taasisi zinazosimamia urasimishaji wa miliki ubunifu kama Brela.
Naye mwakilishi kutoka Shirika la Miliki Ubunifu Kanda ya Afrika (ARIPO), Outle Rapuleng, alisema taarifa zinaonesha kwamba asilimia 95 ya maombi ya kurasimisha miliki ubunifu yanayotumwa kwenye shirika hilo kwa mwaka, yanatoka nje ya Afrika na kwamba ni asilimia tano pekee ya maombi kutoka Afrika.
“Ukiangalia maombi yanayotumwa Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO), yanayotoka Afrika ni asilimia 0.5. Kwa asilimia kubwa maombi ya ulinzi wa IP yanatoka nchi zilizoendelea. Hii ni changamoto ambayo Waafrika tunapaswa kuishughulikia kwa sababu tafiti na bunifu zinafanyika,” alisema.