Shilingi 2.2 bilioni zilizowekezwa kwenye katika mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT- Mifugo na Uvuvi), zimeanza kuzaa matunda baada vijana kupata faida kutokana na uvuvi wa vizimba.
Kikundi cha wajasiriamali wa uvuvi wa samaki kwa kutumia vizimba kinachoitwa Twihame, cha jijini Mwanza kimefanikiwa kuvuna zaidi ya samaki 4,000 katika kizimba kimoja wenye thamani ya Sh. 30 milioni.
Kwa upande wake, kikundi cha Nguvu Kazi kimefanikiwa kupata zaidi ya Sh. 100 milioni, baada ya Septemba mwaka huu, kuvuna samaki waliowafuga kwa njia ya vizimba.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amevipongeza vikundi hivyo sambamba na kumshukuru Rais Samia kwa kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha kufanikisha mradi wa BBR-Mifugo na Uvuvi.
“Inaleta matumaini makubwa sana na mwitikio wa uwekezaji katika Ziwa Victoria kupitia vizimba ni mkubwa na utasaidia kupunguza uvuvi haramu,” amesema Waziri Ulega.
Ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ni miongoni mwa mikakati ya wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya mradi wa BBT, inayolenga kuwainua vijana kiuchumi.
Kwa mujibu wa utafiti wa akiba ya samaki nchini, uliofanyika mwaka wa 2021, inakadiriwa kuwa tani 4,058,914.
Aidha, kiasi hicho hakijumuishi akiba ya samaki katika Ukanda wa Kiuchumi wa Kipekee (EEZ).
Katika utafiti huo, Ziwa Victoria lilitajwa kuwa na akiba kubwa zaidi likikadiriwa kuwa na samaki tani 3,465,914, wa aina mbalimbali wakiwamo sangara na sato; likifuatiliwa na ziwa Tanganyika lenye akiba ya tani 295,000.
Maeneo mengine na idadi ya samaki kwenye mabano ni Nyasa (tani 168,000), eneo la bahari ya Hindi (tani 100,000) na tani 30,000 katika vyanzo vidogo vya maji.
Utafiti huo, umetaja kwamba sekta ya uvuvi ina fursa nyingi ambazo zikitumiwa vizuri ikiwamo ufugaji wa vizimba, zinaweza kubadilisha uchumi wa wananchi wengi ndani ya muda mfupi.