Wajasiriamali katika Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, vimenufaika na mtaji wezeshi wa Sh. 101.6 milioni kutoka benki ya CRDB, kwa ajili ya kuimarisha biashara zao.
Hafla ya kukabidhi hundi hiyo imefanyika jana Septemba 18, kwa vikundi nane na kutoa semina ya kuvijengea uwezo vikundi vya wanawake wajasiriamali na vijana wanufaika wa programu ya Imbeju.
Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe, Dk. Pindi Chana, alifungua mafunzo hayo na kuwataka wanufaika kuitumia fursa zinazotolewa na CRDB kukuza ujasiriamali.
Waziri Chana amesema fursa waliyopata ni mwendelezo wa juhudi za Serikali katika kuboresha biashara za vijana na wanawake, kwa kuweka sera zinazoruhusu uwezeshaji wananchi kiuchumi.
“Uwepo wa CRDB Bank Foundation wilayani Ludewa, ni fursa kwa wanawake na vijana wa Halmashauri hii kuelimika na kuanza kufanya biashara kwa malengo makubwa, yatakayosaidia kukuza kipato cha mtu binafsi, uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla,” amefafanua.
Meneja wa benki ya CRDB, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jenipher Tondi, amesema mafunzo hayo yatasaidia kukuza biashara za wajasiriamali, mitaji na kuimarisha kipato binafsi na kukuza uchumi.
Alisema Imbeju imelenga kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea ustawi wa jamii.
Vikundi vilivyopokea hundi hiyo ni Faraja Luilo, Hope Women Mlangali, Lake Nyasa, Nipende Group, Tupendane Lupanga, Wanawake Luilo, Wanawake Mwangaza Luilo na Mboga Mboga Group.