Wakulima na maofisa ugani kutoka Kata 31 za Muheza-Tanga na Hai na Siha-Kilimanjaro, wamepewa mbinu za kudhibiti wadudu waharibifu wa matunda aina ya parachichi, machungwa na embe, ili kilimo hicho kiwaletee manufaa stahiki.
Mafunzo hayo yametolewa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), kupitia vituo vyake vya Ukiriguru (Mwanza), Tengeru (Arusha) na Mlingano (Tanga), kwa kushirikiana na watafiti kutoka Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Fiziolojia na Ikolojia ya Wadudu (ICIPE), cha Nairobi nchini Kenya.
Watafiti waliwanoa wakulima na maofisa ugani hao katika mafunzo ya siku tano, ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa njia husishi za kudhibiti wadudu wa miti ya matunda kwenye ikolojia mbalimbali.
Taarifa ya TARI imeeleza kuwa katika wilaya za Hai na Siha, mafunzo yalijikita katika matunda ya parachichi, wakati kwa Wilaya ya Muheza mafunzo yalilenga machungwa na embe.
Mtafiti kiongozi kutoka TARI-Ukiriguru, Dk. Abdullah Mkiga, amesema lengo la mafunzo ni kuwapa wakulima elimu bora ya kudhibiti wadudu waharibifu wa matunda kama nzi na nondo, ambao husababisha matunda kuoza na kushusha kiwango cha mavuno na ubora.
Naye mtafiti kutoka ICIPE, Dk. Shepard Ndlela, amesema kupitia njia husishi za kudhibiti visumbufu, mkulima ataweza kupunguza gharama na matumizi ya viuadudu vya kemikali na kuongeza mavuno na ubora kwa soko ndani na kimataifa.
Mradi huu unatekelezwa kwa miaka mitatu (2023-2026), kupitia kituo cha TARI Ukiriguru kwa kushirikiana na taasisi ya ICIPE chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).
Wakulima wa machungwa Kijiji cha Mkinga, wilayani Muheza, Charles Semagongo na Fatuma Muhammed, wamesema mafunzo hayo yamemwezesha kuwatambua wadudu ambao awali walidhani ni hatarishi kwenye matunda.
Aidha, wamesema mafunzo yamewasaidia kutambua pia wadudu rafiki kwenye uzalishaji wa matunda ambao awali wao walidhani ni hatarishi.
Mafunzo hayo yanatolewa chini ya mradi wa njia shirikishi za kudhibiti wadudu wa miti ya matunda kwenye ikolojia mbalimbali.
Dk. Mkiga amesema mafunzo hayo yataleta tija kwa wakulima hasa kujua tabia za wadudu hao pamoja na kuwakabili kuanzia hatua za awali hadi mavuno.
Mradi huo wa miaka mitatu (2023-2026), unatekelezwa na kituo cha TARI Ukiriguru kwa kushirikiana na ICIPE kutoka Nairobi nchini Kenya kwa ufadhili wa GIZ.