WAJASIRIAMALI nchini wametakiwa kuzalisha bidhaa zenye ubora ili waweze kushindana katika soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Afrika na mabara mengine.
Aidha, mashirika ya viwango ya nchi za EAC yameingia makubaliano, ambapo bidhaa ikishathibitishwa ubora na shirika la viwango la nchi husika, haitakiwi kupimwa tena inapopelekwa kwenye soko la nchi nyingine.
Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Ofisa Uthibiti Ubora wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Sileja Lushibika, wakati akitoa elimu kwa wajasiriamali 46 pamoja na wananchi kwenye maonesho ya saba ya mifuko ya programu za kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Maonesho hayo yalifanyika mkoani Singida katika Viwanja vya Bombadier kuanzia Septemba 8 hadi 14, mwaka huu.
“Kupitia maonesho haya tunawaeleza wajasiriamali kwamba kwa sasa tupo kwenye soko la EAC ambapo mashirika ya viwango ya nchi hizo yameelewana kwamba bidhaa zinazozalishwa nchi mojawapo zinaweza kwenda nchi yoyote bila kulazimika kupimwa tena.
“Tunahakikisha wajasiriamali wadogo wanaendelea, serikali inagharamia kuthibitisha ubora wa bidhaa za wajasiriamali na kuendelea kuhudumiwa kwa miaka mitatu tukiwa na imani kwamba baada ya hapo watakuwa wamekua,” alisema Lushibika.
Alisema TBS itaendelea kuhakikisha wajasiriamali wanapata elimu ya kupata alama ya ubora, kwa kuwa upatikanaji wake umerahisishwa.
“Wote walioshiriki maonesho haya wanapokuja hapa wanapata elimu ya namna ya kupata alama ya ubora, tunawapa kanuni bora za usindikaji kwani kuna vitu vya msingi ili bidhaa iweze kuwa bora,” alisema Lushibika.
Alitoa wito kwa wajasiriamali kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ambao ni bure na kwamba utaratibu wa kutuma maombi umerahisishwa, ambapo maombi yanatumwa kwa njia ya mtandao.
Alisema wajasiriamali wanatakiwa kuwa na barua ya utambulisho kutoka Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) wanapowasilisha maombi ya kuthibitisha bidhaa zao.