Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo, amewataka wabunifu wote nchini kulinda bunifu zao kwa kuzisajili kisheria, ili zisichukuliwe na watu wengine na kujinufaisha nazo bila kufuata utaratibu wa kisheria.
Ametoa wito huo wakati wa ziara aliyoifanya ofisi za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), jijini Dar es Salaam ili kujionea utendaji kazi na kujifunza namna wakala inavyotoa huduma.
Amesema kuna bunifu nyingi ambazo zinachukuliwa na watu wengine wanaziendeleza na kujiongezea kipato, bila wabunifu waanzilishi kunufaika na chochote kwa kuwa hawakuzisajili.
“Ninatoa wito kwa Watanzania wabunifu wote kusajili bunifu zenu kupitia BRELA, maana taasisi hii inakazi ya kulinda haki za ubunifu ili kuwawezesha kufaidika na jitihada za ubunifu na hatimaye kuongeza kipato kwa wabunifu na taifa kwa ujumla,” amesisitiza Waziri Jafo.
Waziri Jafo amesema Tanzania imesaini mikataba na nchi mbalimbali katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), pamoja na Soko Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), inayowawezesha Watanzania kunufaika na fursa za biashara.
“Kuna haja ya wabunifu kutambua haki zao ili zisichukuliwe na wenzetu hivyo niwaombe Watanzania kusajili bunifu zao.”
Amewaelekeza watumishi wa BRELA kuwa wawezeshaji wa wafanyabiashara kwa kuwasaidia katika kufanikisha kurasimisha biashara zao na siyo kuwa kikwazo.
Aidha, amewataka kutumia kanuni na sheria kusaidia biashara kwenda mbele na sheria, ambazo zinakwamisha ziwasilishwe ili zifanyiwe maboresho.
“Ni muhimu kuelewa jukumu la BRELA ni kujenga misingi na mazingira mazuri ya biashara.”
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa BRELA, Prof. Neema Mori, amesema wakala umedhamiria kuhakikisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini yanakuwa bora zaidi kwa kuwawezesha, kuwarahisishia na kutoa usaidizi wa karibu kwa wafanyabiashara wanaporasimisha biashara, kutoa elimu pamoja na kuwahusisha wadau mbalimbali ili wajue namna.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, amesema sera ya miliki ubunifu inaelekea kupitishwa na baadae kuwa na sheria, ambayo itasaidia ongezeko kubwa la maombi ya ulinzi wa bunifu hizo ambapo kuna jitihada ambazo BRELA inaendelea nazo katika kuhakikisha elimu ya miliki bunifu inafahamika kuanzia ngazi ya shule ya za msingi hadi vyuo vikuu.
Mbali na jukumu la kusajili miliki ubunifu na utoaji wa hataza, amesema BRELA inatoa ufadhili wa shahada ya uzamili ya Miliki Ubunifu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa watu watano kila mwaka.