Mkurugenzi Mtendaji wa Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC), Mwajuma Hamza, amewataka wanawake na vijana kuchangamkia fursa ya Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), ili wakuze haraka biashara zao.
Ameyasema hayo mkoani Kagera alipokuwa akifungua mafunzo ya taratibu, kanuni na sheria za kufanya biashara katika eneo hilo, yaliyoandaliwa na TWCC kwa kushirikiana na Trade Mark Africa.
Alisema soko hilo linakadiriwa kuwa na watu bilioni 1.3 na kwamba programu nyingine inayotekelezwa na chemba hiyo ni ile ya zabuni (Bid for Success-B4S).
“Kiu yetu ni kuona wanawake na vijana wanafika masoko makubwa, wanapata zabuni za serikali na binafsi na kwenye miradi ya kimkakati kupitia programu yetu ya twende sokoni Afrika na B4S,” amesema.
Akitoa somo katika mafunzo hayo, mkufunzi kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Protaz Lutabala, amesisitiza matumizi salama ya kemikali na kuhimiza matumizi ya vifaa kinga katika uzalishaji.
Lutabala amewataka wajasiriamali kufuata taratibu za usajili wa biashara za kemikali ili kuepuka matatizo ya kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Wajasiriamali pia wameelezwa mbinu za ufungashaji wa bidhaa, upatikanaji wa alama ya ubora na faida na umuhimu wa msimbomilia (barcode) na QR CODE kwenye maduka makubwa kama ‘supermarket.’