WANAWAKE na vijana wameanza kupigwa msasa ili waweze kushiriki zabuni za umma na binafsi, kwa kupewa mbinu za kuandaa nyaraka zinazokidhi taratibu za kisheria wakati wa mchakato wa kuomba kazi au kutoa huduma kwenye taasisi mbalimbali.
Wanawake na vijana 30 wameanza mafunzo hayo katika awamu ya kwanza jijini Dar es Salaam na yanatolewa na Chemba ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC), kwa ufadhili wa TradeMark Africa.
Akifungua mafunzo hayo leo, Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Mwajuma Hamza, amesema: “Tunategemea kuwafikia takribani wanawake na vijana 400 ndani ya miaka mitatu na katika kundi la kwanza tumeanza na 30. Watejengewa uelewa wa kina kuhusu Sheria ya Ununuzi ya Umma, kanuni na mbinu bora za kushiriki katika michakato ya zabuni na jinsi ya kuandaa nyaraka za zabuni zinazokidhi taratibu za kisheria.”
Amesema mafunzo hayo yanalenga kutoa fursa muhimu kwa wanawake na vijana wajasiriamali ambao wanataka kujijenga zaidi katika soko la umma na kukua kibiashara.
“Washiriki watapata faida mbalimbali, ikiwa ni pamoja na elimu ya kina kuhusu masuala ya zabuni na michakato ya kushiriki manunuzi ya umma, ufahamu kuhusu fursa za zabuni na kujengewa uwezo wa kumiliki na kukuza biashara endelevu,” amesema.
Mwajuma amesema wakati wa mafunzo washiriki wataunganishwa na kusajiliwa kwenye mifumo ya kidigitali kwa ajili ya kuona zabuni zinazotangazwa, ikiwemo mfumo wa serikali wa ununuzi ya umma (NeST), mifumo ya Umoja wa Mataifa na sekta binafsi.
“Pia watawezeshwa na kuunganishwa na wataalamu wa kibiashara watakaowasaidia katika mchakato wa kushiriki fursa za zabuni, kuandaa mpango biashara na kuunda wasifu mzuri wa kampuni,” amesema.
Mkurugenzi Mkazi wa TradeMark Africa, Elibariki Shammy, ameipongeza TWCC kwa kuanzisha programu hiyo na amethibitisha kuwa ofisi yake itashirikiana na chama hicho ili kufikia malengo.
Mafunzo hayo yanatolewa ikiwa ni utekelezaji wa programu ya ‘BID FOR SUCCESS’ (B4S), inayolenga kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki zabuni na za binafsi.
Kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi ya Umma (PPRA), sura na 410 ya mwaka 2023 kifungu cha 64, Halmashauri na ofisi zote za serikali, zinapaswa kutenga bajeti yake ya ununuzi kila mwaka kwa ajili ya wazabuni wanawake, vijana na makundi maalumu.
Kanuni za sheria hiyo (PPR), ambazo zimeanza kutumia mwaka huu wa fedha 2024/2025, zinazitaka ofisi za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya makundi hayo.
Trending
- BRELA, UDSM wawanoa wadau faida miliki ubunifu
- Utafiti kilimo, mifugo na uvuvi kutokomeza njaa
- NMB yaja na mwarobaini mikopo kausha damu
- TARI kuzalisha miche 100,000 ya parachichi msimu ujao
- BBT YAANZA KUZAA MATUNDA KWENYE UVUVI
- MAREKANI YATOA BIL 60/- KUIMARISHA USALAMA WA CHAKULA
- BOT YAONYA APP ZA MIKOPO MTANDAONI, YAPIGA MARUFUKU UDHALILISHAJI
- VIJANA, WANAWAKE WAPEWA MITAJI WEZESHI MILIONI 101/-