Na Mwandishi Wetu
Vijana wanaopenda kujiunga na mafunzo ya ufundi wa fani mbalimbali wameitwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kujiunga na vyuo vyake vilivyopo mikoa yote nchini.
Tangazo la VETA limetaja baadhi ya fani za ufundi zinaotolewa ni umeme wa magari (AE), mitambo, majokofu na kiyoyozi, ufungaji umeme, msaidizi wa maabara, Sekretarieti na kompyuta, useremala na uunganishaji, teknolojia ya ushonaji na ubunifu wa mavazi na uashi na ufyatuaji matofali.
Nyingine ni ujenzi na matengenezo ya barabara, uchoraji na uandishi wa alama, uchomeleaji na utengenezaji wa vyuma, teknolojia ya usindikaji wa nyama, mapishi, huduma za chakula na vinywaji na mauzo, utunzaji wa nyumba, ufungaji wa mabomba na ufugaji.
Taarifa imeeleza kuwa serikali inagharimia asilimia 90 ya mafunzo kwenye vyuo hivyo kwa kozi ndefu na asilimia 10 inalipwa na wazazi au walezi wa mwanafunzi.
“Tunakukumbusha kuwa fomu za kujiunga na mafunzo ya muda mrefu kwenye vyuo vya VETA kote nchini zinapatikana. Serikali hugharamia asilimia 90 ya ada na gharama za wanafunzì wanaosoma mafunzo ya muda mrefu katika vyuo vya VETA kupitia Mfuko wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VET Fund),” tangazo la VETA linafafanua.
Mamlaka hiyo inaeleza zaidi kuwa “Chanzo kikuu cha mapato ya mfuko huu ni tozo ya kuendeleza ujuzi (Skills and Development Levy-SDL) ambayo waajiri huchangia.”
Taarifa ya VETA inaonyesha kwamba ada ya sasa kwa kozi ndefu ni Shilingi 60,000 kwa Wanafunzi wa kutwa na Shilingi 120,000 kwa wale wa bweni kwa mwaka; wakati kozi fupi ada yake ikiwa juu.
Aidha, baadhi ya vyuo vya Mamlaka hiyo vinatoa kozi za muda mfupi kuanzia wiki mbili hadi miezi sita katika baadhi ya fani ikiwamo ya udereva wa magari ya abiria, udereva wa magari (awali, VIP-Daraja la kwanza na la pili), ufundi bomba, ushonaji, umeme wa majumbani, uungaji vyuma, uashi, useremala, zana za kilimo (Agro mechanics), ufundi wa magari (Motor Vehicle Mechanics), ufundi umeme wa magari (Auto Electric) na kompyuta.
Nyingine ni mapishi, upambaji wa kumbi za chakula na mikutano, uvuvi na uchakataji samaki, uhazili, utengenezaji wa soseji, ufumaji, huduma kwa wateja (customer care), Kiingereza, ufundi wa marumaru, uchanganyaji wa rangi, udereva wa bodaboda na utengenezaji wake wake.
Nyingine ni kunyoosha mabodi ya magari na kupiga rangi, urembo na ususi, uendeshaji kitalu nyumba, uokaji wa mikate, keki na kuipamba na ufundi aluminiam.
Kwa mujibu wa VETA, baadhi ya vyuo vinavyotoa kozi nyingi na idadi yake kwenye mabano ni Chang’ombe Dar es Salaam (86), Dodoma (44), Mwanza (33), Mbeya (37) na Arusha (14). Aidha, chuo cha Arusha kinatoa kozi nyingi zaidi zinazolenga sekta ya utalii.
“Umri wa kujiunga ni kuanzia miaka 15 na kuendelea, ngazi ya elimu ya msingi na sifa za ziada kwa baadhi ya fani zimebainishwa kwenye fomu ya maombi,” taarifa ya VETA inaeleza.
Trending
- BRELA, UDSM wawanoa wadau faida miliki ubunifu
- Utafiti kilimo, mifugo na uvuvi kutokomeza njaa
- NMB yaja na mwarobaini mikopo kausha damu
- TARI kuzalisha miche 100,000 ya parachichi msimu ujao
- BBT YAANZA KUZAA MATUNDA KWENYE UVUVI
- MAREKANI YATOA BIL 60/- KUIMARISHA USALAMA WA CHAKULA
- BOT YAONYA APP ZA MIKOPO MTANDAONI, YAPIGA MARUFUKU UDHALILISHAJI
- VIJANA, WANAWAKE WAPEWA MITAJI WEZESHI MILIONI 101/-