Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imejipanga kuwasaidia Wajasiriamali nchini kupitia Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa ajili ya Mauzo Nje ya Nchi (ECGS), pamoja Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati (SME-CGS).
Lengo ni kuwezesha wakopaji wenye miradi mizuri, kupata mitaji kutoka kwenye benki na taasisi za fedha, pale wanapokuwa na upungufu wa dhamana ambayo inatoa fursa ya udhamini.
Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane yanayofanyika Nzuguni jijini Dodoma, Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Fedha wa BoT, Gloria Samwel Chellunga, amesema benki hiyo inasimamia mfuko wa udhamini wa mkopo kwa niaba ya serikali ili kuwasaidia Watanzania.
Chellunga amesema mfuko wa udhamini wa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati unawawezesha wenye miradi mizuri lakini wana upungufu wa dhamana, kuweza kupata mitaji kutoka kwenye mabenki na taasisi za fedha.
“Mfuko huu unatoa udhamini usiozidi asilimia 50 kwa mikopo kati ya shilingi milioni 50 hadi shilingi bilioni moja itakayotolewa kwa kipindi kati ya mwaka 1 hadi 5,” amesema.
“Mikopo kwa ajili ya Mauzo Nje ya Nchi umelenga kuwezesha wakopaji wenye miradi mizuri kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa na mauzo nje ya nchi, kupata mitaji kutoka kwenye benki na taasisi za fedha, pale wanapokuwa na upungufu wa dhamana,” amesema Chellunga.
Aidha, ameongeza kuwa udhamini wa mikopo katika mfuko huu hauzidi asilimia 75 kwa mkopo unaolipika ndani ya mwaka mmoja; na asimilia 50 ya mkopo kwa mkopo unaolipika zaidi ya mwaka mmoja.
“Kwa mkopo wa mazao ambayo mzunguko wa uzalishaji na uuzaji wake unazidi miezi 12 lakini si zaidi ya miezi 15, udhamini wa mkopo hautazidi asilimia 75,” ameongeza.
Amesema kuwa lengo ni kusaidia sekta binafsi pamoja na wajasilimali wadogo wenye miradi mzuri na kupata mikopo kutoka benki au taasisi za fedha zinazosimamiwa na benki kuu ambao wamepungukiwa na dhamana.
Amefafanua kuwa ili uweze kupata dhamana katika mifuko huo, mwombaji ambaye ni mjasiliamali mdogo akiwemo mvuvi au mkulima, anatakiwa kutuma maombi katika benki yake akiwa na andiko linaloelezea mradi wake.
Amefafanua kuwa benki itafanya tathmini ya mkopo huo kwa kuzingatia sera na benki husika itatuma maombi BoT kwa ajili ya kupata dhamana kwa ajili ya kumkopesha mteja wake.