WANAWAKE, Vijana na wenye mahitaji maalumu wameshauriwa kujiunga na mfumo wa manunuzi ya umma (National e-Procurement System of Tanzania-NeST), ili waweze kuona zabuni za umma mara tu zinapotangazwa na kuziomba.
Akizungumza kwenye mkutano wa asubuhi (breakfast meeting), ulioandaliwa na Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), na kuwakutanisha wanawake na vijana zaidi ya 300, Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Kanda ya Pwani, Vicky Mollel, amesema wanawake wana nafasi ya kukuza biashara zao kupitia miradi ya serikali kwa njia ya zabuni.
Amesema ili kushinda zabuni, ni muhimu kwa wanawake kujisajili kwenye mfumo wa NeST, ili watambulike na waweze kuona zabuni pindi zinapotangazwa.
“Wote mnafahamu kwamba bajeti ya serikali mwaka huu wa 2024/2025 ni Sh. trilioni 49.3, asilimia 70 ya bajeti hii itatumika katika ununuzi kupitia sheria ya ununuzi wa umma…PPRA inashirikiana na TWCC katika kuhakikisha makundi maalum kama vijana, wanawake, wazee na watu wenye mahitaji maalum wanapata nafasi katika fursa za ununuzi wa umma. Kwa mfano, wanawake wana fursa ya kupata asilimia 10 ya zabuni kupitia asilimia 30 ya bajeti ya manunuzi inayotengwa kwa makundi haya maalum,” amesema.
Amesema wanawake wakichangamkia fursa hiyo na kufanikiwa kufanya biashara na serikali, itawasaidia kukuza haraka biashara zao na hivyo kukuza uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Mwajuma Hamza, amesema chemba hiyo inalenga kuwezesha wanawake na vijana nchini kuzijua fursa na kuzichangamkia.
Amesema mbali ya mtaji wa fedha, biashara zinahitaji mtandao wa taarifa za masoko, teknolojia ya uzalishaji pamoja fursa za kukua zaidi.
“Tumekuwa na mikutano hii ya asubuhi kila mwezi lengo ni kujenga mtandao wa kibiashara, kukutana na wadau wanaowapa fursa wanawake, taarifa na ujuzi ili wafanye maamuzi sahihi katika kukuza biashara zao. Leo tumewaalika watu wa PPRA ambao wameeleza namna ambavyo tunaweza kufanya biashara na serikali,” amesema.
Kadhalika, amesema wanawake na vijana wana nafasi ya kuchangamkia soko kubwa la kimataifa (EACLC), Ubungo ambalo litakuwa na maduka zaidi ya 2,000.
Rais wa chemba hiyo, Mercy Silla, amewataka wanawake wachangamkie fursa hizo na kujitokeza kwa wingi ili kufaidika na zabuni za umma zinazopatikana.
Pia amewashauri waingie kwenye soko la EACLC ambalo linaweza kuwaunganisha na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali nchini China, wakiwamo wa mashine, ambazo zinahitajika na wanawake wazalishaji.
Kwa mujibu wa Silla, mkutano huo wa asubuhi ulilenga kuwajengea wanawake na vijana uwezo katika masoko na biashara, kuunda mitandao ya kibiashara na kuelewa soko kubwa la Afrika Mashariki na kufunguliwa kwa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCTA).
Meneja Uendeshaji wa kampuni ya PASS, Neema Nyangalamela, amesema wanawake na vijana walio kwenye mnyororo wa kuongeza thamani mazao ya kilimo na mifugo, wanaweza kukopa vifaa na mashine, kuanzia za maandalizi ya shamba, kuvuna na kuzalisha bidhaa kwa ajili ya mlaji wa mwisho.
“Kwenye sekta ya uvuvi tunatoa mkopo wa vifaa kwa wale wanaohusika na mazao yanayolimwa baharini, wafugaji wa wanyama mbalimbali kama kuku, samaki na ng’ombe, wazalishaji wa asali na wamiliki wa mazao ya misitu,” alisema.
Amesema tayari wanawachama wa TWCC wameshapatiwa vifaa vyenye thamani ya Sh. milioni 50.
Naye Ofisa Masoko wa mfuko wa uwekezaji wa pamoja (UTT), Pili Kunambi, alisema Watanzania wanaweza kuwekeza na kupata faida kila mwezi katika mfuko huo.
Trending
- BRELA, UDSM wawanoa wadau faida miliki ubunifu
- Utafiti kilimo, mifugo na uvuvi kutokomeza njaa
- NMB yaja na mwarobaini mikopo kausha damu
- TARI kuzalisha miche 100,000 ya parachichi msimu ujao
- BBT YAANZA KUZAA MATUNDA KWENYE UVUVI
- MAREKANI YATOA BIL 60/- KUIMARISHA USALAMA WA CHAKULA
- BOT YAONYA APP ZA MIKOPO MTANDAONI, YAPIGA MARUFUKU UDHALILISHAJI
- VIJANA, WANAWAKE WAPEWA MITAJI WEZESHI MILIONI 101/-