Na Mwandishi Wetu, Morogoro
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), umetahadharisha matumizi ya ‘vishoka’ kusajili kampuni, huduma au majina ya biashara, kwa kuwa wengi hutumia taarifa za wahusika vibaya.
Akiwasilisha mada kwenye mafunzo ya waandishi wa habari za biashara yanayofanyika mjini hapa, Meneja katika sehemu ya makampuni BRELA, Lameck Nyangi, amesema huduma za taasisi hiyo zinapatikana kwa urahisi kwa njia ya mtandao (ORS), ambao unamlazimu mhusika kujisajili kwa jina lake ili aweze kuhudumiwa.
“Unakuta mtu anarahisisha tu mambo, anamtafuta mtu anamwambia amsajilie kampuni hadi anampa taarifa zake muhimu wala hajishughulishi kujua ni namna gani mfumo unafanyakazi, matokeo yake sasa kishoka anatumia uzembe wa mhusika anajiingiza kuwa sehemu ya kampuni, mtu anaanza kufanyabiashara pasipokujua kwamba kuna mmiliki asiyehusika,” amesema.
Nyangi ameongeza: “Kwa hiyo pale unapotaka kufanya mabadiliko au maboresho kwenye nyaraka ulizowasilisha BRELA mwanzoni, huwezi kufanya hivyo bila yule kishoka. Wakati mwingine unakuta kampuni imepata faida, unashangaa kunaibuka mgogoro na mtu ambaye ni mmiliki wa kampuni ambaye humjui.”
Amesema kosa lingine linalofanywa na watu wanaosajili kampuni ni kuingiza wabia kishkaji ili kutimiza takwa la kisheria, jambo ambalo linasababisha migogoro pindi mafanikio ya kibiashara yanapoanza kutokea.
“Unakuta umepata ‘dili’ ambalo linakutaka uwe na kampuni, unaona kwa haraka haraka umwingize mshkaji wako, unampa na umiliki wa hisa zilizolipiwa, huyo uliyemwingiza hakusaidii chochote, matokeo yake baada ya muda unapata faida ya Sh. milioni 600, anaibuka kudai gawio,” amesema.
Amesema sheria ya kampuni sura ya 212 inataka kampuni isajiliwe na walau wanahisa wawili, lakini inasisitiza muungano wa hiari wenye malengo ya kufanya biashara, uwekezaji au kutoa huduma kwa ajili ya kupata faida.