“Tiba shufaa ni maalumu kwa ajili ya kuimarisha maisha ya mgonjwa, kimwili, kiakili na kiroho ili aweze kuishi vizuri wakati wote wa kuugua,” anasema.
Na Restuta James
UKIKUTANA naye huwezi kudhania kwamba ni mtu mwenye changamoto ya maradhi. Sura yake yenye nuru na ukaribisho wa tabasamu ni vitu vitakavyokuhakikishia kuwa Jasmin Said Salum ni mwanamke mwenye maisha ya kawaida kama wengine.
Jasmin shujaa wa saratani mwenye miaka 33, alibainika kuwa na maradhi hayo miaka mitatu iliyopita na kukatwa titi moja.
Akizungumzia safari yake ya ugonjwa hadi kuwa shujaa, Jasmin anasema siku moja aliona ana uvimbe kama gololi kifuani ambao hakikuwa kinauma.
“Nilivyokiona sikuridhika nacho, kesho yake nikaamkia zahanati ambako daktari aliniandikia dawa za wiki mbili za kuyeyusha uvumbe. Wiki ya tatu nikasikia kitu kinaniambia hebu minya chuchu nilivyominya nikaona inatoa majimaji ambayo ni mazito kama rangi ya mafuta ya kula,” anasema.
Jasmin anasema kadri siku zilivyozidi kuendelea, chuchu ilianza kutoa damu ambayo ilimshtua japokuwa hakuwaza kama inaweza kuwa ni saratani.
“Nilihisi kile kiuvimbe kilikuwa ni jipu kwa hiyo limepasukia kwenye ziwa, hata sikurudi hospitali. Ziwa likaendelea kutoa damu hata bila kukamuliwa nikafikia hatua ya kulala na brazia; nikiamka imelowa, nikiingia bafuni kuoga damu zinatoka, hii hali sikuridhishwa nayo, mwenzangu (baba mtoto wake), akaniambia niende hospitali,” anasema.
Anasema alienda hospitali ya Mkoa Temeke ambako baada ya vipimo alibainika kuwa na uvimbe ambao madaktari walimshauri afanyiwe upasuaji, tiba ambayo haikumridhisha kwani mwenza wake alitafuta taarifa za dalili za saratani na kumshauri kwenda Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).
Jasmin anasema baada ya wiki moja alienda Ocean Road alikofanyiwa vipimo na baada ya vipimo, dakari alimrudisha Temeke kwa barua ya maombi ya kumkata kinyama ili kifanyiwe uchunguzi wa kina katika hospitali ya Taifa Muhimbili na majibu yarudishwe ORCI.
“Nilifanya kama daktari alivyoelekeza…sikusomewa majibu Muhimbili, nilivyoyapokea niliyapiga picha nikawatumia baadhi ya madaktari ambao wengine walinificha, daktari mmoja mwanamke nilimuomba aniambie ukweli, akaniambia Jasmin una saratani naomba kesho uende Ocean Road,” anasema.
Jasmin anaongeza kuwa: “Nilishtuka na kulia sana sikuamini. Nikampigia simu mwenzangu kumpa majibu, akakata simu akaniambia anakuja. Nililia nikijua maisha yangu ndio basi tena. Namshukuru Mungu mwenzangu alinipa moyo sana, hadi niliamka pale kama siumwi.”
Anasema kesho yake aliamkia ORCI ambako daktari alimsomea majibu na kumthibitishia kuwa anayo saratani. Anasema hakutetereka kwa kuwa alishafanyiwa unasihi nyumbani.
“Madaktari waliitana kama watatu hivi, wakaniangalia ziwa na kunishauri nikatwe kwa sababu kwa umri wangu ugonjwa ungesambaa sana. Hili lilinishtua mno kwa sababu sikutegemea kabisa kukatwa ziwa,” anasema.
Jasmin mama wa mtoto mmoja mwenye miaka sita, anasema alirudi nyumbani akiwa mnyonge na aliyepoteza tumaini lakini mwenzi wake alimsihi kukubali tiba hiyo kwani wako watu wanaopoteza viungo vikubwa zaidi ya titi.
Jasmin anasema safari yake ya tiba ilianza rasmi Juni 14, 2022 alipokatwa titi katika hospitali ya Taifa Muhimbili na baada ya wiki moja alihamishiwa ORCI.
“Nikaanza mzunguko wa chemo (tiba kemia), nikaingia kwenye mionzi na sasa ninatumia dawa za homoni. Namshukuru sana Mungu naendelea vizuri,” anasema.
Hata hivyo, anasema tiba kemia ilimsababishia kutapika kupita kiasi hadi familia ilimzuia kuendelea nayo lakini walivyompa nafasi ya kuamua, aliomba arudishwe Ocean Road.
“Namshukuru Mungu nilimaliza chemo zote nane nikaingia kwenye mionzi ambayo nilipiga 16, nilipata vidonda lakini nilipambana mpaka nikamaliza matibabu na Februari mwakani nitatimiza miaka miwili tangu nilipomaliza matibabu,” anasema Jasmin.
Anasema alipomaliza tiba mionzi alianza kutumia dawa za kurekebisha homoni ambazo anaendelea nazo huku akihudhuria kliniki katika taasisi hiyo.
Shujaa mwingine wa saratani ya matiti aliyekatwa titi la kushoto, Stella Mbonde, anasema aligundulika kuwa na maradhi hayo miaka 22 iliyopita na kueleza kuwa saratani inatibika kama itagundulika katika hatua za awali.
Stella anawasihi wananchi kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara ili iwe rahisi kubaini ugonjwa mapema kabla haujasambaa na kushindwa kutibika.
ORCI NA TIBA SHUFAA
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo ya saratani nchini, Dk. Julius Mwaiselage, anasema mbali ya tiba za kisayansi, hospitali inatoa tiba shufaa inayoundwa na daktari, muuguzi, mfamasia, ustawi wa jamii, mwanasaikolojia, mtaalamu wa lishe na watu wa huduma za kiroho.
“Tiba shufaa ni maalumu kwa ajili ya kuimarisha maisha ya mgonjwa, kimwili, kiakili na kiroho ili aweze kuishi vizuri wakati wote wa kuugua,” anasema.
Dk. Mwaiselage anafafanua tiba shufaa inaambatana na utoaji wa dawa ya maumivu aina ya Oral Morphine, inayomwondolea maumivu mgonjwa wa saratani aliye katika hali ya juu ya ugonjwa.
“Kubwa katika tiba shufaa ni utoaji wa dawa za maumivu, tunafahamu wagonjwa wengi hasa wa muda mrefu wanapata maumivu na ndicho kinachofanya maisha ya mgonjwa yasiwe bora. Oral Morphine ni maalumu kabisa kuondoa maumivu ya aina yoyote,” anasema.
Anasema kabla ya mgonjwa kupewa dawa hiyo, huanza na dawa za awali ambazo zisipopunguza maumivu kwa kiwango kinachotakiwa, huanza dozi hiyo.
Dk. Mwaiselage anasema ORCI, inatoa dawa hiyo kwa kuwa wagonjwa wengi wa saratani wanafika hospitali wakiwa katika hatua za juu za ugonjwa inayoambatana na maumivu makali.
“Moja ya jukumu la tiba shufaa ni kuhakikisha mgonjwa hapati maumivu, kwa hiyo dawa maalum ipo kama nilivyosema na tunaitoa kwa wagonjwa wenye uhitaji huo,” anasema.
Anasema taarifa za jarida la kiutafiti la Lancet lilieleza kuwa takribani watu milioni 25 walifariki mwaka jana wakiwa katika maumivu makali; na kwamba Oral Morphine inalenga kuhakikisha mgonjwa hapati maumivu hata anapokuwa katika hatua za juu za ugonjwa.
Anasema kwa mwaka ORCI inahudumia wagonjwa 65,000 ambapo mwaka jana 46,061 kati yao waliingia kwenye mpango wa tiba shufaa.
Anasema asilimia 60 hadi 70 ya wagonjwa walifika kwenye taasisi hiyo wakiwa katika hali ya juu ya ugonjwa na kwamba ndio maana wametoa kipaumbele cha dozi ya Oral Morphine.
Kwa mujibu wa daktari huyo, dawa hiyo inaweza kutolewa kwa wagonjwa wa ajali, kisukari na akili; walio katika maumivu makali.
Daktari bingwa wa saratani, Dk. Faraja Kiwanga, anasema mbali ya tiba shufaa, hospitali hiyo inatibu saratani kwa mionzi, kemia, upasuaji, vichocheo na dawa za kupunguza maumivu.
Mkurugenzi wa uuguzi na muuguzi bingwa wa tiba shufaa, Mary Haule, anasema wagonjwa wengi wa saratani wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo za kisaikolojia wakihofia tiba na uwezekano wa kupona.
“Kuna wengine ni vijana, wengine ni wazazi ambao wana wategemezi nyuma yao. Wengi wanapopata saratani wanajiuliza nimemkosea ni Mungu ndio maana kwenye tiba shufaa tunakaa nao kuwaweka sawa,” anasema.
“Kwenye tiba shufaa tunaanza kumhudumia tangu anapopokea majibu ya ugonjwa, tunampa faraja kwa lengo la kuboresha maisha ya mgonjwa na familia yake,” anasema.
Kwa mujibu wa ORCI, saratani inayoongoza nchini na asilimia yake kwenye mabano ni ya shingo ya kizazi (35), matiti (15), njia ya chakula (10), ngozi (9), muunganiko wa saratani ya kichwani, mdomoni na shingoni (8), tezi dume (7) na utumbo mpana (6).