SERIKALI inakusudia kuweka huduma za mtandao yaani WiFi katika uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maboresho makubwa yanayotarajiwa kufanyika katika uwanja huo.
Lengo la huduma hiyo ni kuwawezesha mashabiki kupata huduma ya mtandao bure wanapokuwa uwanjani hapo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Saidi Yakubu, ameyasema hayo mkoani Njombe wakati akifungua kikao kazi cha 14 kwa maofisa maendeleo utamaduni na maofisa maendeleo ya michezo wa mikoa yote ya Tanzania bara.
“Tunakwenda kushirikiana na wenzetu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari watatuwekea mfumo wa WiFi pale bure utakuwa ukiingia uwanjani kuangalia mpira unapata free WiFi,” amesema Yakubu.
Yakubu amegawa mipira 54 kila mkoa ambapo mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Ally Mayai, amesema mipira hiyo ni sehemu ya maandalizi ya Samia Taifa CUP yatakayofanyika Oktoba, mwaka 2023.