UPATIKANAJI wa uhakika wa gesi, mafuta maalumu ya kupikia (bioethanol), mkaa na kuni mbadala ndilo suluhisho la uharibifu wa mazingira na kupunguza athari za mbadiliko ya tabia nchi, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji ya Maendeleo (UNCDF), limesema.
Ofisa Mwandamizi wa masuala ya fedha wa UNCDF na Meneja wa mradi wa Cookfund, Imanuel Muro, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi alipokuwa akizindua kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ya ‘Anzia Jikoni-mabadiliko ya hewa safi ya baadae yanaanzia jikoni.’
Alisema ili kuwezesha upatikanaji wa nishati safi, Umoja wa Ulaya (EU), umetenga EURO milioni 17 (takribani Sh. bilioni 47.6), kwa ajili ya kufadhili kampuni na wajasiriamali wanaojihusisha na uzalishaji na usambazaji wa nishati safi.
“Huwezi kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa bila kuleta mabadiliko ya nishati ya kupikia. Ufadhili wa EU unalenga ubunifu wa teknolojia ya kisasa ya kupata majiko yanayotumia mkaa, gesi na kuni kidogo. Tunatoa ruzuku kwa kampuni ili mtumiaji wa mwisho aweze kupata nishati na jiko kwa bei ndogo,” alisema.
Muro alisema ufadhili huo unalenga kusaidia biashara ya nishati safi ya kupikia ambayo ni rafiki wa mazingira, ili kuchangia juhudi za kidunia za maendeleo endelevu na kuokoa mazingira.
Alisema kampeni ya ‘Anzia Jikoni’ inalenga kuueleza umma umuhimu wa matumizi ya teknolojia za kupikia zinazopunguza madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
Muro alitaja baadhi ya teknolojia ambazo zimeshavumbuliwa kwa ajili ya kupikia kuwa ni mkaa na kuni mbadala, majiko ya gesi yanayotumia kiasi kidogo cha nishati hiyo, mafuta (bioethanol) kwa ajili ya kupikia na jiko la umeme linalotumia umeme kidogo.
Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa mradi wa Cookfund, Elizabeth Ngoye, alisema ndani ya miezi mitatu, watumiaji wapya 3,373 wamefikiwa na nishati safi ya kupikia, katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma na Mwanza, inayohusika kwenye mradi huo.