RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema visiwa hivyo vina nafasi ya kuendelea kushirikiana na Serikali ya Ujerumani kwenye uwekezaji katika sekta ya utalii.
Ameyasema hayo leo Juni 8, 2023 alipozungumza na Balozi wa Ujerumani, Regine Hess, ambaye amemaliza muda wa utumishi wake nchini Tanzania.
Rais Mwinyi amesema Ujerumani imetoa mchango mkubwa visiwani hapa kupitia sekta ya majisafi na salama, ambayo aliieleza kuwa muhimu kwa ustawi wa wananchi wa Zanzibar.
Ameishukuru serikali ya Ujerumani kwa ushirikiano wanaoutoa kwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia sekta za afya na michezo, pamoja na kushajihisha watalii raia wa nchi hiyo, kutembelea vivutio vya Tanzania.
Balozi Hess amempongeza Rais Mwinyi kwa kuridhia serikali ya umoja wa kitaifa pamoja na uamuzi wa kuunda kamati ya maridhiano ya kitaifa kati ya CCM na ACT Wazalendo.
Kadhalika, Balozi Hess amemtambulisha balozi wa heshima, Dk. Jenny Bouraima, atakayeiwakilisha Ujerumani visiwani hapa.
Dk. Jenny ameahidi kushirikiana na serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika nyanja ya utalii na kuunga mkono sera ya uchumi wa buluu kwa kuwahamasisha Wajerumani kuwekeza visiwani humo kupitia rasilimali bahari.