SERIKALI ya Norway imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kupitia Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), katika miradi mbalimbali ukiwamo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Balozi wa Norway nchini, Elisabeth Jacobsen, ameyasema hayo alipotembelea SUA na kuona miradi ya ushiriki wa vijana kwenye kilimo.
Amesema kwa zaidi ya miaka 50, Tanzania na Norway zimekuwa na uhusiano mzuri hivyo anakusudia kuendeleza ushirikiano huo kwa kuanzisha na kuendeleza miradi ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi hususani hewa ukaa.
“Norway pia kuna mambo mengi ya kushirikiana… hatutashiriki kwenye kilimo pekee bali hata kwenye masuala ya miradi ya mabadiliko ya hali ya hewa,” amesema Balozi Elisabeth.
Makamu Mkuu wa SUA, Profesa Raphael Chibunda, amesema ujio wa balozi huyo ni sehemu ya kudumisha ushirikiano baina yao.
“Norway ndiyo iliyotusaidia kuanzisha Ndaki ya Misitu, Ndaki ya Uzalishaji wa Wanyama vilevile hivi karibuni wametusaidia kuanzisha kituo cha hewa ukaa katika miaka 50 iliyopita kwa nyakati tofauti walitusaidia kugharamia miradi mbalimbali ya tafiti,” amesema Profesa Chibunda.
Mmoja wa wahitimu wa SUA ambaye ni mkulima katika kituo atamizi chuoni hapo, Happiness Nyanga, amesema atatumia maarifa na ujuzi alioupata chuoni hapo katika kutimiza malengo yake ya kuwa mkulima mkubwa wa mazao ya mboga na matunda.