RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Ikulu mjini Unguja mapema leo.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Charles Hillary, kwa vyombo vya habari imesema kwamba viongozi hao wamezungumzia ustawi wa Zanzibar kisiasa na kijamii.
“Viongozi hao wameafikiana kwamba ipangwe tarehe ya kuzindua rasmi kamati maalumu itakayoundwa na wajumbe kutoka CCM (Chama Cha Mapinduzi) na ACT-Wazalendo, ambavyo ndivyo vilivyounda serikali ya Umoja wa Kitaifa, kuanza kujadiliana na baadae kupanga mpango wa utekelezaji wa ripoti ya kikosi kazi kilichoundwa,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Imefafanua kuwa viongozi wa ACT-Wazalendo waliokutana na Rais Mwinyi ni Mwenyekiti Juma Haji Duni, Makamu Mwenyekiti ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Othman Masoud na Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe.