UGONJWA wa saratani umeendelea kuwa tishio kwa wanawake kutokana na sababu kadhaa ikiwamo kutonyonyesha ipasavyo, kuchelewa kupata mtoto na kutopata chanjo kwa wakati.
Takwimu za Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), za Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu, zinaonyesha kwamba, Tanzania inapata wagonjwa wapya 42,046 kila mwaka na miongoni mwao ni asilimia 44 ya wanawake wanaokabiliwa na saratani ya mlango wa kizazi.
Mkurugenzi Mkuu wa ORCI, Dk. Julius Mwaiselage, anasema saratani ya shingo ya kizazi ni tatizo kubwa na imeendelea kuongezeka siku hadi siku.
Anasema wanawake walio kwenye hatari ya kupata aina hiyo ya saratani ni wale wenye wapenzi wengi na wale ambao hawajapata chanjo.
“Kila mwanamke au msichana ana vimelea vya saratani, huwa vinapotea lakini wengine huwa vinashamiri kutokana na kuanza ngono mapema, kuwa na wapenzi wengi na kutokupata chanjo,” anasema.
Anasema mbali ya shingo ya kizazi, wanawake wanakabiliwa na saratani ya matiti ambayo inashika nafasi ya pili kati ya 10 zinazowashambulia wananchi.
Anasema aina hiyo ya saratani imeongezeka hadi kufikia asilimia 17, ikifuatiwa na ya njia ya chakula kooni (asilimia 12).
Anataja aina nyingine za sarataji na asilimia zake kwenye mabano kuwa ni ya kichwa na shingo (9), ya ngozi (6), tezi dume (5), thyroid (3), utumbo mpana (2), lymphoma (1) na ya damu (1).
Anataja njia mojawapo ya kujikinga na saratani ni chanjo, ambayo inatolewa kwa watoto wenye umri wa miaka tisa hadi 14; na kwamba mwanamke akishavuka umri hawezi kupata chanjo hiyo.
Badala yake, Dk. Mwaiselage anashauri kwamba wanawake wenye zaidi ya miaka 14, wawe na desturi ya kupima afya mara kwa mara, ili ikibainika kuwa na tatizo hilo waweze kupata tiba mapema.
Kwa mujibu wa taarifa za ORCI, visababishi vikubwa vya saratani ya kichwa na shingo, ni matumizi ya tumbaku yaani sigara na ugoro, unywaji wa pombe kupita kiasi, usafi wa kichwa usioridhisha na unene kupita kiasi.
Kadhalika, saratani ya koo inasababishwa na matumizi ya sigara na ugoro. Saratani ya matiti ambayo inawaathiri zaidi wanawake, inasababishwa na kutokunyonyesha kikamilifu au kutonyonyesha kabisa na kuchelewa kupata mtoto.
Aidha, visababishi vya jumla vya saratani kwa mujibu wa taasisi hiyo, ni unene uliopitiliza, kutokula matunda na mbogamboga, kutofanya mazoezi, kutofanya uchunguzi wa awali, matumizi ya tumbaku, mwanga wa jua kwa wenye ualbino na unywaji pombe kupita kiasi.
Anashauri wananchi kuwa na desturi ya kufanya mazoezi walau kwa dakika 30 kila siku na kutoka jasho, kula mboga na matunda, kupunguza matumizi ya nyama nyekundu, kutumia nafaka zisizokobolewa na kula maharage na vyakula jamii ya mikunde.
Dk. Mwaiselage anasema uchunguzi wa ugonjwa wa saratani hadi tiba, unagharimu fedha nyingi ambazo zinalipwa kwa sehemu kubwa na serikali.
Anasema mgonjwa mmoja ana gharimu Sh. milioni tatu, kiasi ambacho ni kikubwa kwa kuwa wagonjwa wengi hawana uwezo wa kumudu kulipa.
“Familia nyingi zenye wagonjwa wa saratani huathirika zaidi kwa sababu hulazimika kusafirisha wagonjwa wao kutoka sehemu ya mbali hadi Taasisi ya Ocean Road,” anasema.
Anaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa ndani ya miaka miwili, ORCI imeanzisha huduma za wodi ya wagonjwa mahtuti (ICU), yenye vitanda 24, uchunguzi wa MRI na digital x-ray pamoja na huduma za tiba mtandao, zinazowafikia wananchi wengi.
“Uanzishwaji wa huduma hizi umetokana na fedha za UVIKO-19 kutokana na mkopo wa masharti nafuu wa IMF…Taasisi inakamilisha usimikaji wa mashine za PET/CT na Cyclotron,” anasema Dk. Mwaiselage.
Dk. Mwaiselage anafafanua kuwa saratani ni ugonjwa unaotibika kama mgonjwa atawahi hospitali mapema na kushauri watu waweke utaratibu wa kupima afya mara kwa mara.
Kutokana na gharama kubwa za matibabu, Mkurugenzi huyo anaomba Watanzania na wadau wengine, kuiunga mkono serikali kwa kuchangia hospitali hiyo ili iweze kuwatibu wagonjwa wanaosumbuliwa na tatizo hilo.
Ombi hilo linaungwa mkono na machifu ambao wanadhamiria kuanzisha mchezo wa mpira wa miguu kwa ajili ya kuchangisha Sh. milioni 300.
Mwenyekiti wa machifu, Antonia Tomisiza, anasema machifu kupitia programu ya Chifu na Huduma Jamii, inakusudia kuchangisha kiasi hicho ili kisaidie matibabu ya wagonjwa 100.
Anasema kiasi hicho cha fedha kitagharimia huduma anazopaswa kupewa mgonjwa kuanzia kumwona daktari, uchunguzi bobezi wa maabara, radiolojia, tiba mionzi na tiba kemia.
“Programu hii itagarimia wagonjwa 100 kwa kipindi ambacho mgonjwa atapokelewa hospitalini hadi atakapoondoka baada ya uchunguzi na tiba,” anasema.
Ili kufanikisha azma hiyo, Chifu Antonia anasema wanakusudia kuwa na mchezo wa mpira wa miguu kati ya machifu vijana na wabunge, utakaochezwa katika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma, Mei 27, mwaka huu.
Anasema mchezo huo utaenda sambamba na ule wa pete wa machifu wanawake vijana dhidi ya wabunge wanawake, nia ikiwa ni kuwaunganisha viongozi wa mila na desturi na wawakilishi wa wananchi.
Mbali ya michezo hiyo, wananchi mkoani Dodoma, watapata nafasi ya kufanyiwa uchunguzi wa magonjwa yasiyoambukiza ukiwamo wa saratani, kuanzia Mei 25 had Mei 28, 2023.
“Ni wajibu wa jamii kufanya kila linalowezekana kuwasaidia wenye changamoto ili kupunguza ugumu na machungu wanayopitia. Programu ya Chifu na Huduma Jamii imekuja kuhamasisha jamii katika kusaidia huduma mbalimbali ambazo serikali inazichukua kukabiliana na magonjwa ya saratani,” anasema Chifu Antonia.
Anaongeza kuwa: “Tunawaomba wadau mbalimbali kuunga mkono programu hii ili kuweza kufikia lengo lililokusudiwa.”