DAKIKA mbili na sekunde 14 tangu walipoanza kuonyesha ufundi wao wa kucheza muziki, watoto wa ‘mtaani’ kutoka jiji la Kampala Uganda, zilitosha kumnyanyua jaji Bruno Tonioli, ambaye aliwapa alama ya dhahabu kwa burudani waliyokuwa wanaitoa.
Hawa si wengine bali ni kundi la Ghetto Kids, linalolelewa na mwalimu Dauda Kavuma, ambaye anawachukua kutoka mitaani wengine wakiwa yatima au kukosa malezi; na hivyo kuwapa malezi pamoja na huduma zote muhimu.
Watoto hawa wamefanikiwa wateka mioyo ya takribani mashabiki 2,286 waliokuwa wanafuatilia onyesho la vipaji la Britain Got Talent, wakati wa kurekodiwa katika ukumbi wa Palladium, jijini London, nchini Uingereza wiki mbili zilizopita.
Wakieleza historia yao, wanasema kuwa ni watoto wa ‘mitaani’ ambao wamepata bahati ya kumpata baba (Mwalimu Kavuma), ambaye anawapa malazi, malezi, chakula na kulipa ada na matibabu pale wanapougua.
Historia hii iliibua sii tu simanzi katika ukumbi wa Palladium bali machozi ya furaha, watu wengi wakimpongeza mlezi huyo anayekuza vipaji vya watoto kwa namna ya pekee.
Jaji Aleshi Dixon, anampongeza Kavuma kwa kumwambia kwamba: “Unafanya kazi nzuri sana, Mungu akubariki mpenzi.”
Baada ya historia fupi iliyoonyeshwa kwa mashabiki wa onyesho hilo, ndipo Ghetto Kids, walipopewa uwanja wa kuonyesha kipawa chao.
Hapa ndipo walipocheza wimbo wa Kiafrika ambao kabla haujaisha, Bruno alilazimika kubonyesha kitufe cha ‘Golden Buzzer’ na kuwamwagia vitu vya dhahabu, ishara kwamba wanachokifanya ni cha thamani ya dhahabu.
Hili halikuwasimamisha madansa hawa na hata mdundo wa wimbo ulipobadilika haukubadilisha stepu zao.
Pamoja na nyimbo nyingine, Ghetto Kids walicheza kwa ustadi mkubwa wimbo rasmi wa Waka Waka, wa Shakira ulioimbwa kwenye mashindano ya kombe la dunia yaliyofanyika Afrika Kusini mwaka 2010.
UMAARUFU WA GHETTO KIDS
Kwa mara ya kwanza walipata kutambulika duniani kote mwaka wa 2017, kwa video ya wimbo wa Afro house unaoitwa Marimba Rija wa mwanamuziki wa Angola Dotorado Pro, ambayo ilitazamwa na watu milioni 25 wakati huo.
Aidha, video ya onyesho lao la London ambalo imewekwa mtandaoni wiki mbili zilizopita, imeshatazamwa na zaidi ya watu milioni 10, ambao milioni 6.7 kati yao wameangalia kupitia chaneli ya Britain Got Talent katika mtandao wa Youtube.
Video hiyo ya Ghetto Kids imepata maoni 13,421 kwenye chaneli hiyo yenye wafuasi milioni 19.4, duniani wengi wakiwapongeza watoto pamoja na mlezi wao.
Ni wazi kwamba rekodi ya kutazamwa na watu milioni 25 itavunjwa ndani ya mwezi mmoja, kutokana na hadhira kubwa waliyoifikia kwa kushiriki mashindano makubwa ya vipaji ya London.
MAONI TOKA KWA MAJAJI
Jaji Kiongozi wa onyesho hilo kubwa duniani, Simon Cowell, ambaye anaonekana kuwa ‘mtata’, aliwapongeza watoto hao akisema wamewapa burudani ya kipekee.
Hata hivyo, anasema kitufe cha Golden Buzzer hubonyezwa baada ya washiriki kuhitimisha onyesho lakini kwao imekuwa pekee kwani wamepata ‘ushindi’ katikati ya shoo.
Anawaambia kuwa anatamani kuwaona kwenye raundi inayofuata, jambo linaloamsha shangwe toka kwa watazamani waliohudhuria onyesho hilo.
Kwa upande wake, Amanda Holden, aliwapongeza watoto hao na kuwaambia wanachokifanya ni cha kibabe.
“Ninyi nyote ni nyota. Tunayoheshima kubwa kwa kuja kwenu kwenye onyesho letu la vipaji,” anasema.
Jaji Tonioli hakuwa na mengi ya kusema baada ya Ghetto Kids kuhitimisha shoo yao na badala yake aliwaambia anatamani kuwaona tena kwenye raundi inayofuata.
GHETTO KIDS NI AKINA NANI?
Ghetto Kids ni sehemu ya familia ya watoto 30 wanaolelewa na mwalimu Kavuma.
Taasisi yake inatoa malazi, chakula na elimu kwa watoto kutoka mitaa ya Kampala tangu 2007. Triplets Ghetto Kids ilisajiliwa kama shirika lisilo la kiserikali miaka 10 iliyopita, kufuatia mafanikio yao ya kucheza muziki na video ya dansi iliyotengenezewa nyumbani ya Sitya Loss na msanii maarufu wa Uganda Eddy Kenzo. Taasisi hiyo hutumia muziki, kucheza au kudansi na maigizo kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kupata maisha bora.
Wameshinda tuzo nyingi za kucheza muziki kimataifa tangu 2015, zikiwamo Afrimma, ambayo ni kubwa kutoka Muungano wa Sekta ya Kurekodi Marekani na Tuzo ya Watayarishi wa YouTube. Walicheza pia kwenye mashindano ya Kombe la Dunia la mpira wa miguu kwa wanaume mwaka 2022.
Marimba Rija ilikuwa chaguo bora kuwaelezea Ghetto Kids, ambao ulitayarishwa na mwanamuziki mashuhuri wa Afro house na nyota wa kuduro.
Kuduro ni aina ya muziki na dansi uliokuwa unatengenezwa Luanda, Angola mwishoni mwa miaka ya 1980. Video hiyo ilihusisha vipengele mahususi vya kucheza kitamaduni na kuongeza miondoko ya asili iliyotokana na ubunifu na mtindo wa kikundi hicho.
Triplets Ghetto Kids ni kielelezo cha haja ya kubadilisha udhaifu wa kihistoria kuwa nguvu kwa jamii nzima. Wanacheza kwa ajili ya elimu na kuendelea kuishi na watafanikiwa.
Wanacheza nyimbo mbalimbali na kutoa video kwenye mitandao ya YouTube, Instagram na TikTok.
Kama mtaalam wa jinsi mitindo ya dansi ya Kiafrika inavyosambaa ulimwenguni kote, nimekuwa nikivutiwa na jinsi maonyesho yao ya kipekee yanavyotokana na nyimbo maarufu za Kiafrika na aina za uchezaji za kitamaduni za Kiafrika – zikiendana na mabadiliko ya kisasa. Ghetto Kids ni uthibitisho wa namna kucheza muziki kunavyoweza kubadilisha maisha.
UPEKEE WA GHETTO KIDS
Mchanganyiko wa mila na ubunifu unasimamiwa kikamilifu na Ghetto Kids. Hatua zao za kimaadili zinaonyesha ushawishi wa kisanii na kitamaduni uliopo kati ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kundi hili pia linafahamu uwezo wa kuonyesha na kuondoa taswira potofu za Afrika kupitia tafsiri za kushangaza na za kuchekesha zitokanazo na ushawishi wao.
Picha ya kijiji cha jadi cha Kiafrika, mandhari ya vijijini na hata ya mitindo ya Kiafrika (kuvaa kofia na koti za kifahari), hutumiwa kuonyesha muonekano wao na mtazamo wao kwenye maisha.
Kujiamini, mbwembwe na matumaini yenye furaha hujionyesha kwenye video na maonyesho yao yote. Wanajikubali jinsi walivyo na wako tayari kushiriki furaha yao pamoja.
Mwanzilishi wa Ghetto Kids, Dauda mara nyingi ameeleza historia yake kwamba na yeye alikuwa mtoto wa mitaani, ambaye hakuwa na uwezo wa kwenda shule, hadi alipokutana na msamaria mwema ambaye alifadhili elimu yake.
Msaada huo ulimfanya aweke nadhiri ya kusaidia wengine na alianza kutengeneza msingi huo baada ya kuhitimu mafunzo ya ualimu (mwalimu wa hisabati).
Imeandikwa kwa msaada wa mtandao.