Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega.
WAFUGAJI kote nchini wametakiwa kutenga maeneo ya malisho katika msimu huu wa mvua kwa ajili ya matumizi wakati wa kiangazi, ili kuepuka migogoro baina yao na wakulima.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia wizi wa Mifugo nchini, ACP Simon Pasua, aliyasema hayo jana wilayani Monduli, alipokutana na viongozi wa wafugaji pamoja na wakulima, kwa lengo la kupanga mikakati ya pamoja ya kuepusha migogoro ambayo imekua ikijitokeza wakati wa kiangazi.
Kamanda Pasua alibainisha kuwa wakati wa kiangazi kunakuwa na ukame hivyo kukosekana sehemu za malisho, hali ambayo inasababisha baadhi ya wafugaji kupeleka mifugo sehemu ambazo sio rasmi.
Pia aliwataka kupanga matumizi bora ya ardhi, pamoja na kuacha kupelekea mifugo kwenye vyanzo vya maji ili kuepuka migogoro na kuvikausha vyanzo hivyo.
Kwa upande, Julius Mariki, kiongozi wa wafugaji katika kijiji cha Mungere, alishukuru ujio wa kikosi hicho na kuomba vikao zaidi ili kuondoa migogoro.
Mkulima Anthony Mroso, wa Kijiji cha Majengo, wilayani Monduli, aliiomba serikali kuainisha maeneo ya kilimo, makazi na malisho.