Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya kuangalia namna ya kuboresha mifumo ya hakijinai nchini, Jaji Mkuu Mstaafu, Othman Mohamed Chande.
Na Restuta James
MALEZI duni, umasikini utandawazi na makundi rika, yanasababisha watoto kufanya makosa makubwa ya kijinai kama mauaji na kufanya unyang’anyi kwa kutumia silaha, ili kupata mahitaji muhimu.
Meneja wa mahabusu ya Watoto jijini Dar es Salaam, Darius Damas, ameiambia Tume ya Kuangalia namna ya Kuboresha Mifumo ya Hakijiani inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Othman Mohamed Chande, ilipotembelea mahabusu hiyo leo.
Amesema mashtaka yanayowakabili watoto ni mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha, ulawiti na ubakaji, matusi, dawa za kulevya na kukutwa na nyara za serikali.
“Kwa ujumla wanakabiliwa na makosa ya mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha; japokuwa na mengine yapo na katika makosa hayo wanakiri na kukutwa wametenda kweli,” amesema Damas.
Damas amesema kosa lingine ni kuishi nchini bila kibali, ambalo linalowakuta watoto wanaosafirishwa kwa njia haramu, wakitokea nchi jirani.
“Malezi duni ndio changamoto kubwa inayosababisha haya yote na single parenting (malezi ya mzazi mmoja). Tunaona kwamba mtoto akipendwa na akapata malezi stahiki anaweza kubadilika na kuwa mwema kabisa. Tunaamini nyumbani ndiyo sehemu nziri zaidi kwa watoto,” amesema.
Amefafanua kuwa makosa ya ubakaji na ulawiti kwa watoto yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na utandawazi, kwa kuona kwenye televisheni.
Damas amesema makosa yote wanayofanya watoto yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na malezi duni, yanayompa mtoto nafasi ya kuangalia vipindi visivyofaa kwenye televisheni, kujiunga na makundi rika yasiyo na maadili, ukosefu wa mahitaji muhimu unaomsukuma kuiba na kujaribu mambo mapya kama ulawiti.
Aidha, amesema watoto wanaofikishwa mahabusu hiyo wanapata nafasi ya kurekebishwa tabia kwa kupewa ushauri na unasihi kutoka kwa maofisa ustawi wa jamii, michezo na burudani, kufundishwa ufundi stadi na kazi za mikono pamoja na elimu ya msingi kwa watu wazima, kwa walio na umri wa zaidi ya miaka 14.
Hata hivyo, amesema kituo hicho kinakabiliwa na uchakavu mkubwa wa miundombinu, uhaba wa vitendea kazi kama gari na bajeti ndogo ikilinganishwa na mahitaji.
Awali, Tume hiyo ilitembelea Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini, ambako Mkuu wa Chuo hicho, Lazaro Mambosasa, amesema kinachofanyika sasa ni kukipanua na kuboresha mitaala ili iweze kuendana na dunia ya sasa.
Amesema pia wapo kwenye hatua za kuanzisha kituo cha utafiti ili iwe rahisi kufanya maboresho yanayohitajika kwa wakati.
Amesema hivi sasa chuo kipo kwenye mazungumzo na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ambayo inategemea kujipanua na kuchukua eneo hilo na kwamba chuo kimejipanga kuhamia kwenye eneo lingine kubwa.
Tume hiyo pia ilitembelea gereza la Segerea, Ukonga, Chuo cha Taaluma ya Urekebu cha Jeshi la Magereza Ukonga, Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, vituo vya polisi vya Buguruni, Mabatini, Kawe na Mahakama ya Watoto Temeke.