Na Restuta James
UWEKEZAJI uliofanywa na Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika bandari ya Dar es Salaam, umeiongezea uwezo na sasa inategemea kuhudumia zaidi ya tani milioni 20 za shehena mchanganyiko kwa mwaka.
Tangu Rais Samia aiingie madarakani, ameshatoa zaidi ya Sh. bilioni 573 ili kuwekeza katika Bandari ya Dar es salaam ikiwamo ununuzi wa mitambo ya kisasa ya kupakua na kupakia makontena.
Ni katika uwekezaji huo ambao umewezesha bandari nzima kufungwa kamera, ili kudhibiti wizi na kuhakikisha usalama wa shehena inayohudumiwa na bandari ya Dar es Salaam.
Lengo la uwekezaji huo ni kuchochea kasi na ukuaji uchumi, ambapo takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 40 ya mapato yatokanayo na kodi yanatokana na shughuli za bandari.
Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es salaam, Mrisho Suleiman Mrisho, ametangaza mafanikio hayo wakati akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa kituo cha utangazaji cha Uhuru FM waliotembelea kujionea maboresho ya bandari ya Dar es salaam.
Kwa mujibu wa Mrisho, uduni wa miundombinu bandarini hapo ilikuwa ni kikwazo na hiyo wamemshukuru Rais Samia kwa uwekezaji huo mkubwa.
Aidha, Bandari ya Dar es salaam, hivi sasa ina uwezo wa kuhudumia meli ya ukubwa wa aina yoyote na kwa wakati wowote, hii ikitokana na maboresho yaliyofanyika ikiwemo ujenzi wa gati mpya namba ziro yenye uwezo wa kuegesha shehena ya magari zaidi ya 6,000 kwa wakati mmoja.
Chini ya maboresho hayo, bandari ya Dar es salaam imekuwa ikihudumia pia mteja mpya ambaye ni nchi ya Zimbambwe, ambapo bidhaa kubwa ya Zimbabwe inayopita katika Bandari hiyo ni magari.
HALI YA ULINZI
Akizungumzia ulinzi na usalama bandarini hapo, Mrisho alisema umeimarishwa zaidi hiyo hakuna wizi wa mafuta wala mizigo.
Alisema maeneo yote ya bandari yamefungwa kamera za kisasa zaidi ya 470, sambamba na uwepo vyombo vya ulinzi, hivyo kuifanya kuwa salama wakati wote.
MELI KUCHELEWA
Alismea hali hiyo imepungua akitoa mfano kwamba ndani ya siku 17, bandari hiyo imehudumia meli kubwa 50 na kwamba lengo ni kuhudumia meli 100 ifikapo mwisho wa mwezi huu.
“Kumekuwa na ongezeko kubwa sana la meli zinazotia nanga bandarini ikiwamo meli kubwa ya watalii zaidi ya 400 kutoka Marekani,” alisema Mrisho.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Uhuru FM, Amina Aziz, amesema kujionea shughuli zinazofanywa na Bandari ya Dar es salaam kumetoa fursa ya kuona namna Serikali ilivyowekeza na kutoa nafasi ya kuwaelimisha wananchi kuhusu bandari hiyo inavyofanya kazi na mafanikio yake.