Na Restuta James
UTAFITI wa kitabibu umeongeza matumaini katika vita dhidi ya Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi (VVU), baada ya kuja na dawa kinga zinazoweza kumkinga mtu asiambukizwe virusi hivyo.
Wataalamu wa afya wametaja dawa kinga hizo kuwa ni pete kinga inayowekwa ukeni na nyingine ni dawa ya sindano anayochomwa mtu kumkinga ndani ya miezi miwili.
Akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mtendaji Mkuu taasisi isiyo ya kiserikali ya DARE Tanzania, Dk. Lilian Mwakyosi, alisema pete kinga ni miongoni mwa njia salama na rahisi kutumia ili kujikinga na VVU hususani kwa wasichana na wanawake kwa ujumla.
Alisema pete hiyo inayojulikana kwa jina la kitaalamu ‘Dapivirine Vaginal Ring (DVR)’, imewekewa dawa maalumu ya kuzuia maambukizi ya VVU, yanayoweza kumpata mwanamke wakati wa kujamiiana.
Alisema DVR ni kinga mahsusi kwa wanawake kwa kuwa inawapa uhuru wa kuamua kujikinga bila kuhitaji ruhusa ya mwenza, kwa kuwa wakati wa kujamiiana mwanaume hawezi kuhisi utofauti.
“Hii ni miongoni mwa njia ya kukabiliana na VVU iliyoidhinishwa hivi karibuni na Shirika la Afya Duniani (WHO), ikijumuisha pete ya ukeni, vidonge na sindano. Njia hizi zinakuja kuziba pengo lililokuwepo katika kujikinga…wote tunahitaji kujikinga lakini tuna mahitaji tofauti,” alisema Dk. Lilian.
Dk. Lilian alisema njia hizo zinakwenda sambamba na nyingine zilizokuwepo awali ikiwamo kuepuka ngono zembe, kutumia kondomu na dawa za kufubaza VVU kwa wale ambao wameshabainika kupata maambukizi.
Alisema sindano, vidonge na pete ya ukeni ni matokeo ya tafiti za kitabibu zinazoendelea duniani, katika kukabiliana na VVU.
Alisema pete hiyo ina dawa ambayo inaweza kukabiliana na VVU ndani ya siku 28 na kwamba mtumiaji anapaswa kuitoa na kuweka nyingine baada ya siku hizo ikiwa atahitaji kufanya hivyo.
“Hii ni njia inayoongezeka ili kukabiliana na VVU na itasaidia sana wanawake ambao hawawezi kutumia njia zilizopo sasa ambazo nyingine zinahitaji maamuzi ya mwenza. Inaongeza nguvu kwa mwanamke kuweza kuwa na uchaguzi wa kujilinda,” alisema.
Alisema tafiti zaidi zinaendelea kufanyika duniani ili kupata tiba kamili ya ugonjwa huo na kuwasihi Watanzania kuendelea kujikinga na kutumia dawa zilizopo ili kuepuka maambukizi.
Kwa upande wake, Mratibu wa asasi ya COMPASS nchini, Francis Luwole, alisema sindano inamchanganyiko wa dawa mbili zinazodhibiti kuzaliana kwa VVU pale vinapoingia kwenye mwili ambao umetumia dawa hiyo.
Alisema tofauti na pete, sindano inakaa mwilini kwa miezi miwili na kwamba baada ya muda huo, mtumiaji anaweza kuchoma tena ili kujikinga.
Hata hivyo, alisisitiza kwamba dawa hiyo haimzuii mtu kuendelea kujilinda kwa kuacha ngono zembe na kwamba hazizuii magonjwa mengine ya zinaa.
“Siku hizi utakuta vijana wanatembea na dawa za kuzuia mimba sio kondomu…hili ni jambo la hatari na inatuthibitishia kwamba elimu zaidi inahitajika kutolewa ili vijana waweze kujikinga dhidi ya VVU na magonjwa mengine ya zinaa,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya mratibu wa masuala ya ukimwi katika Manispaa ya Kinondoni, Dk. Amos Kitonga, alisema takwimu zinazonyesha kwamba asilimia 95 ya Watanzania wamepima VVU na kwamba asilimia 98 ya waliobainika kuwa na maambukizi wanatumia ARV.
Alifafanua kuwa vifaa vya kupimia VVU vinapatikana nchi nzima kuanzia zahanati, ikiwa ni mpango wa serikali kurahisisha upimaji na ushauri nasaha kwa wananchi.
Mtendaji Mkuu wa Asasi isiyo ya kiserikali Mulika Tanzania, Hussein Melele, alisema vyombo vya habari vina nafasi ya pekee ya kuendelea kuhabarisha umma kuhusu VVU na Ukimwi, kwa kuwa Tanzania ina idadi kubwa ya vijana.
Hata hivyo, dawa kinga hizo bado hazijaidhinishwa kutumika nchini. Kwa Afrika, zimeidhinishwa Kenya, Uganda, Rwanda, Zimbabwe na Afrika Kusini, ambako zimeanza kutumika.